TFRA YAKUTANA NA WADAU KUTATHMINI MPANGO WA MBOLEA YA RUZUKU

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent akizungumza na waingizaji na wazalishaji wa mbolea nchini( hawapo pichani) katika kikao maalum cha kufanya tathmini ya utekelezaji wa Mpango wa Ruzuku kwa msimu wa kilimo 2023/2024 tarehe 14 June, 2024
Wadau wa mbolea wakifuatilia mahojiano katika kikao cha kutathmini utekelezaji wa Mpango wa ruzuku kwa msimu wa kilimo 2023/2024 baina yao na TFRA tarehe 14 Juni, 2024
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) akiongoza kikao baina yake na wadau wa mbolea kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Mamlaka Jijini Dar Es Salaam tarehe 14 June, 2024

....................

Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) imefanya mkutano na wazalishaji pamoja na wafanyabiashara wa mbolea nchini ili kutathmini mwenendo mzima wa tasnia ya mbolea hususani utekelezaji wa mpango wa utoaji wa mbolea za ruzuku katika msimu wa 2023/2024.

Katika mkutano huo wadau hao wa mbolea wamejadili masuala mbalimbali katika tasnia ya mbolea yakiwemo mafanikio yaliyopatikana katika msimu wa kilimo wa 2023/2024.

Akizungumza wakati wa kikao hicho Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent amekiri kuridhishwa na utekelezaji wa Mpango wa Ruzuku ya Mbolea ulioanza kutekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita mwaka 2022/23.

Mkurugenzi Laurent ameyasema hayo hivi karibuni alipokuwa akizungumza na Waingizaji na Wazalishaji wa mbolea wa ndani ya nchi katika kikao kilichofanyika katika Ofisi za Mamlaka Jijini Dar Es Salaam.

Aidha, Mkurugenzi Laurent aliwashukuru wadau kwa namna wanavyounga mkono juhudi za Serikali katika kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mbolea kwa kuanzisha mashamba ya mfano katika maeneo mbalimbali nchini na kutoa huduma ya kupima afya ya udongo kwa wakulima ili kuwawezesha kutumia mbolea kulingana na mahitaji ya undongo na zao lililolimwa.

Akitaja mafanikio mengine katika utekelezaji wa Mpango wa Ruzuku amesema mtandao wa usambazaji wa mbolea umeongezeka na mfumo wa kidijitali wa utoaji na uuzaji wa mbolea za ruzuku umeimarika na kuwezesha na kurahisha usambazaji nchini.

Akizungumzia kikao hicho, Claudia Kimako, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara na Masoko wa Itracom amesema ni kikao cha kawaida kinacholenga kutoa mwanga wa namna nzuri ya kuanza msimu kwa kuondoa changamoto zilizobainika katika msimu unaoisha na kubaini fursa kwa msimu unaofuata.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mbolea Tanzania (TFC) Samuel Mshote amesema katika msimu wa 2024/2025 wataagiza na kuÅŸambaza kwa wakulima jumla ya tani 150,000 za mbolea za kupandia na kukuzia yenye ruzuku ya Serikali.Katika msimu ujao Mshote ameongeza kuwa TFC itanza uwekezaji katika ujenga wa kiwanda cha kuchanganyia mbolea chenye uwezo wa kuchanganya tani 120 kwa Saa.

" Katika msimu ujao tutakarabati maghala ya kuhifadhi mbolea yaliyopo Mbeya, Makambako Tabora, Mwanza, Sumbawanga na Songea na kuwa ya kisasa", Alisema Mshote.

Kwa mujibu wa Mshote katika msimu ujao TFC itaongeza mtandao wa mawakala wa usambazaji kutoka mawakala 400 Mpaka 1000. 

0/Post a Comment/Comments