********
Shirika la Reli Tanzania (TRC) limesema safari za treni ya kisasa (SGR) kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro zitaanza Ijumaa ya Juni 14, 2024.
Hayo yamesemwa leo Jumatano Juni 12, 2024 na Mkurugenzi Mkuu wa TRC, Masanja Kadogosa wakati wa kampeni ya uzinduzi wa huduma za uendeshaji wa SGR, iliyopewa jina la “Twende tupande treni yetu, tuitunze, tuithamini.”
Kadogosa amesema mwanzo wa safari hizo ni ishara ya kuimarika kwa miundombinu ya usafirishaji, itakayochochea ukuaji wa uchumi wa kanda.
Amesema TRC imeanza na Dar es Salaam- Morogoro kama hatua ya awali zitakazowezesha kupata uzoefu na kutatua changamoto zitakazojitokeza, ili kuboresha safari zitakazoendelea.
Hata hivyo safari hizo za treni zitaanza ikiwa ni mwezi mmoja kabla ya muda ambao Rais Samia mwaka jana aliiagiza TRC kuhakikisha treni hizo zinaanza kusafirisha abiria kuanzia Julai mwaka huu.




Post a Comment