VGS 135 KUONGEZA NGUVU MAPAMBANO DHIDI YA WANYAMAPORI WAKALI NA WAHARIBIFU

............,......

Na. Sixmund Begashe

Wizara ya Maliasili na Utalii inaendeleza mkakati kabambe wa kupambana na Wanyamapori wakali na waharibifu pamoja na kuimarisha uhifadhi kwa kutoa Mafunzo kwa Askari Wanyamapori wa Vijiji (VGS) 135.

Akifunga mafunzo ya Askari hao Katika Chuo Chuo Cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii (CBCTC)Likuyu Sekamaganga, Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed amesema utoaji wa Mafunzo hayo kwa VGS ni jitihada  za Serikali chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuwalinda wananchi dhidi ya  Wanyamapori wakali na waharibifu pamoja, kuendeleza Uhifadhi wa rasilimali na Kukuza sekta ya Utalii nchini. 

Mhe. Ahmad ameongeza kuwa jitihada hizi za Mhe Rais Samia zinapaswa kuungwa mkono kikamilifu na Wahitimu hao kwa kuyatimia Mafunzo waliyoipata kwa weledi mkubwa na kwa malengo yaliyokusudiwa na si vinginevyo. 

“Askari 108 mliopata mafunzo ya Askari Wanyamapori wa Vijiji zingatieni kuwa Taifa linawategemea ili mkaongeze nguvu kazi katika ulinzi wa rasilimali za maliasili na hasa kudhibiti wanyamapori wakali na waharibifu katika jamii zenu.”  Alisisitiza Mhe Ahmad

Aidha Mhe. Ahmad amewataka wahitimu  hao kuwa waalimu wazuri kwenye jamii zao  kwa kuwafundisha mbinu za kudhibiti wanyamapori kwa kutumia mbinu ambazo ni rafiki katika mazingira yao ili jamii nzima iweze kuzitumia na hivyo kupunguza changamoto hiyo.

Kwa upande wa askari wahitimu 27 waliopata mafunzo ya Utalii na uongozaji watalii, Ahmed aliwaasa kufanyakazi kwa weledi katika maeneo yao ili kuhamasisha utalii wa ndani na wa nje na hivyo kuongeza idadi ya watalii nchini.

Mhe. Ahmed aliwasihi kutumia vizuri mbinu walizojifunza za ujasiliamali katika sekta ya utalii, kwa kuanzisha miradi mbalimbali midogo midogo ya kuwaingizia kipato ili waweze kujiajiri, kujiongezea kipato na hivyo   kunufaika na elimu waliyoipata.

Katika  kuzingatia mpango wa matumizi bora ya ardhi katika maeneo yaliyopo jirani na hifadhi, mapito na mtawanyiko wa wanyamapori, Mhe Ahmad ametoa rai kwa wananchi kujiepusha na tabia ya kufanya Shughuli za kijamii kwenye maeneo yaliyohifadhiwa kisheria pamoja na  kupiga wanyamapori wakali kwa kutumia silaha mbalimbali za kimila/jadi pindi wanapoingia kwenye maeneo ya wananchi. 

Akizungumzia Mipango ya Wizara katika kuboresha mazingira ya utoaji melimu katika Chuo hicho, Mkurugenzi wa Kitengo cha Utafiti na Mafunzo, Wizara ya Maliasili na Utalii Dkt. Edward Kohi amesema pamoja na mambo mengine,  Wizara imeandaa mpango wa kuwapatia Mafunzo watumishi wa Chuo hicho Katika ngazi mbalimbali za elimu, pamoja na kuhakikisha kinakuwa na kituo cha afya.

Akitoa taarifa ya Mafunzo hayo, Mkuu wa  Chuo cha Mafunzo ya Uhifadhi wa Maliasili kwa Jamii (CBCTC) Likuyu Sekamaganga,  Bi Jane Nyau, amebainisha kuwa Kati ya askari 136 walioanza mafunzo Machi 3, 2024 ni askari 135 waliohitimu mafunzo kati ya hao askari 108 ni wa kozi ya VGS na 27 ni wahitimu wa kozi ya muda mfupi ya Utalii na Uongozaji Watalii huku askari mmoja akishindwa kuhitimu kutokana na utovu wa nidhamu.

Bi Nyau ameongeza kuwa askari  83 wakiwemo VGS  56 na kozi ya Utalii na Uongozaji watalii 27 (REGROW), VGS 50 wamefadhiliwa na Shirika la  GITZ kupitia mradi wa kuzuia migongano baina ya binadamu na wanyamapori na  VGS 2 kwa ufadhili wa Shirika la Wildlife Conservation Society (WCS).


 

0/Post a Comment/Comments