*******
Na Tausi Mbowe
TMDA yaonya matumizi holela ya dawa hizo
Matumizi makubwa na holela ya dawa za Viuajisumu yanaelezwa kuongezeka nchini hasa wakati wa kipindi cha mlipuko wa ugonjwa wa Covid (Uviko-19).
Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa matumizi hayo kwa kiasi kikubwa yameleta madhara kwa wananchi.
Moja ya madhara hayo ni pamoja na usugu wa vimelea vya magonjwa dhidi ya dawa (AMR) na kuwa tishio kwa afya si kwa Tanzania pekee bali duniani kote kwa kukwamisha matibabu ya maambukizo ya vimelea vya maradhi.
Takwimu zilizotolewa na TMDA za mwaka 2018 hadi 2021 zilizochapishwa hivi karibuni kuhusu utafiti uliofanyika kufuatilia mwenyendo wa matumizi ya dawa za Viuajisumu nchini Tanzania kabla na baada ya mlipuko wa ugonjwa wa Uviko-19 zinaonyesha kwamba kumekuwa na onhgezeko la asilimia 21 ya dawa hizo.
Kwa mujibu wa TMDA, wakati wa uwepo wa ugonjwa huo wa Uviko-19 miongoni mwa dawa za Viuajisumu zilikuwa na ongezeko kubwa ni pamoja na dawa ya Gentamicin, Azithromicin na tetracycline.
Hata hivyo, TMDA inasema katika kipindi hicho cha mliouko wa ugonjwa wa Uviko-19 ilibaini kwamba matumizi ya dawa aina ya Chloramphenicol na Norfloxacin yalipungua.
TMDA inasema inaendelea kufuatilia matumizi ya dawa hizo ikiwa ni pamoja na kutosajili dawa za kundi hilo ambazo zimeshindwa kutibu kutokana na usugu.


Post a Comment