**********
📌 Ampongeza Dkt. Biteko
kwa kuiongoza vyema Wizara na TANESCO kwa utekelezaji wa miradi
📌 Akagua vituo vya
kupoza umeme Nguruka na Kidahwe
📌
Aagiza ifikapo Septemba Kigoma iwe imeingia kwenye Gridi ya Taifa
📌 Kapinga asema Wizara
haitakuwa kikwazo cha wananchi kupata umeme wa uhakika
Makamu wa Rais, Mhe. Dkt Philip Isdor Mpango ameipongeza Wizara ya Nishati kwa usimamizi
madhubuti wa miradi mbalimbali ya Sekta ya Nishati hususan miradi ya umeme
ambayo inapelekea nchi kuzidi kujiimarisha kiuchumi.
Dkt. Mpango ametoa pongezi hizo leo leo Julai 8, 2024
wakati alipokagua utekelezaji wa
mradi wa ujenzi wa njia kuu ya kusafirisha umeme wa msongo wa Kilovoti
132 kutoka Tabora hadi Kigoma yenye urefu wa Kilomita 395 pamoja na ujenzi wa
kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme cha Nguruka na na Kidahwe
vilivyoko mkoani Kigoma.
Akiwa kwenye kituo cha kupoza umeme cha Nguruka ambacho
ujenzi wake umefikia asilimia 95, Dkt. Mpango ameiagiza Wizara ya Nishati
kupitia TANESCO kuhakikisha ifikapo mwezi Septemba mwaka huu Kigoma iwe
imeungwa kwenye Gridi ya Taifa ya umeme na hivyo kutatua changamoto ya
upatikanaji wa umeme ambao umekuwa ukirudisha nyuma shughuli za uwekezaji
kwenye mkoa huo.
‘’Nimpongeze Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.
Doto Biteko kwa kuisimamia vyema sekta hii, na pia niwapongeze sana TANESCO kwa
kazi nzuri mnayofanya ila ni muhimu sasa
mkahakikisha Mkoa wa Kigoma unaingia kwenye Gridi ya Taifa ili
kuufungua mkoa huu kiuchumi."
Amesema Dkt Mpango
Kwa upande wake,
Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga amemshukuru Makamu wa Rais, kupitia Serikali
inayoongozwa na Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutenga fedha za kutosha
kuwezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali hususan mradi wa ujenzi wa kituo cha
kupoza umeme cha Nguruka na kuahidi kuendelea kusimamia miradi ya nishati ili
kuhakikisha umeme unapatikana kwa uhakika kwa wananchi.
‘’ Nikuhakikishie Mhe Makamu wa Rais sisi Wizara ya Nishati
tunakuhakikishia kuwa hatutakuwa kikwazo kwa wananchi kupata umeme bali
tunaahidi kuwapatia umeme wa uhakika watanzania wote’.’ Amesema Mhe Kapinga
Ameongeza kuwa Wizara itaendelea kutekeleza miradi ya umeme
ya kimkakati ikiwemo ujenzi wa mradi wa umeme wa Igamba Kidahwe hadi Malagarasi
ambapo mpaka sasa mkandarasi ameshakabidhiwa eneo la mradi.
Mradi wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa kilovoti 132
kutoka Tabora hadi Kigoma na kituo cha kupoza umeme cha Nguruka unatekelezwa na
mkandarasi kampuni ya TBEA kutoka China
na unagharimu kiasi cha zaidi ya shilingi
bilioni 12 na ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Kidahwe kitakachopokea umeme kutoka Nyakanazi
unagharimu shilingi bilioni 5 na unatekelezwa na wataalam wa ndani
kutoka TANESCO.
.Ujenzi huo ukikamilika utaunganisha Wilaya nne za Mkoa wa Kigoma ambazo ni Kigoma Mjini,
Buhigwe, Uvinza na Kasulu na pia kuongeza hali ya upatikanaji wa umeme kwa mkoa
wa Kigoma kupitia Gridi ya Taifa.
Post a Comment