FAIDA AHUKUMIWA JELA NA KULIPA FIDIA YA MIL. 3 KUMKATA VIGANJA MAMAKE MDOGO CHATO*

 

 Jengo la Mahakama ya wilaya ChatoMonica Laurent Nonga,akionyesha jinsi alivyojeruhiwa baada ya shambulio lililo fanywa na nduguye.

.............
 Na Daniel Limbe,Chato

MAHAKAMA ya wilaya ya Chato Mkoani Geita imemhukumu Faida Enocka(26) kifungo cha miaka minne jela na kulipa fidia ya shilingi milioni 3 baada ya kupatikana na hatia ya kumkata viganja vya mikono mama yake mdogo,Monica Laurent Nengo, na kumsababishia ulemavu wa kudumu kutokana na imani za kishirikina.

Uamuzi huo umetolewa na Hakimu mfawidhi wa mahakama ya wilaya hiyo ,Erick Kagimbo,baada ya kusikiliza maelezo na ushahidi wa pande zote mbili uliowasilishwa mbele ya mahakama hiyo.

Katika kesi hiyo namba 757 ya mwaka 2023 ilikuwa ikisimamiwa na Jamhuri chini ya mwendesha mashitaka wa polisi,Mauzi Lyawatwa,ambapo imetamatika baada ya mshitakiwa kupatikana na hatia ya kutenda kosa la kujeruhi kinyume cha sheria za nchi.

Awali mwendesha mashitaka huyo, aliieleza mahakama kuwa mnamo julai 20, 2022 majira ya saa mbili usiku mshitakiwa alimshambulia mama yake mdogo kwa kitu chenye ncha kali kutokana na imani za kishirikina kisha kumsababishia majeraha ya kudumu.

Hata hivyo baada ya kutambua kuwa ametenda ukatili huo alikimbia kwenda kujificha kwa lengo kukwepa mkono wa sheria na baada ya kukamatwa na jeshi la polisi alifikishwa mahakamani Oktoba 26, 2023.

Lyawatwa amesema kitendo hicho cha kujeruhi ni kinyume na kifungu cha sheria namba 225 cha mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 16 kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022 huku akiiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa.

Hata hivyo, kabla ya kutolewa hukumu hiyo, mshitakiwa amepewa nafasi ya kujitetea ili kupunguziwa adhabu, ambapo amesema ana watoto pamoja na mama yake mzazi ni mlemavu na wote wanamtegemea pia kwa kuzingatia kuwa amekaa gerezani muda mrefu anaiomba mahakama hiyo imwonee huruma.

Akisoma hukumu hiyo,Mheshimiwa Kagimbo, amesema kutokana na ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashitaka na kwa kuzingatia utetezi wa mshitakiwa mwenyewe, mahakama hiyo imejiridhisha pasipo shaka kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo kinyume cha sheria za nchi.

Na kwamba kwa kuzingatia maelekezo ya sheria za nchi, mahakama hiyo imeamua kumhukumu kifungo cha miaka minne jela, na kumlipa Monica fidia ya shilingi milioni 3 ili iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hizo.

Aisha mshitakiwa amechukuliwa chini ya ulinzi wa polisi na kupelekwa gereza la wilaya ya Chato kuanza kutumikia adhabu yake.

0/Post a Comment/Comments