(PICHA NA MPIGAPICHA WETU)
Ofisi ya Makamu wa Rais kupitia Mradi wa Urejeshwaji
Endelevu wa Mazingira na Hifadhi ya Bayoanuai Tanzania (SLR) imetenga ekari
28,000 za misitu ya jamii iliyopo katika vijiji vya Halmashauri saba (07) kwa
ajili ya urejeshaji wa uoto wa asili.
Hayo yamebainishwa Julai 31, 2024 Mkoani Iringa na
Mratibu wa Kitaifa wa Mradi wa SLR, Dkt. Damas Mapunda wakati wa mahojiano na
waandishi wa vyombo vya habari katika kikao cha siku moja cha kamati ya kitaifa
ya usimamizi wa mradi kilichopokea taarifa ya mradi huo.
Dkt. Mapunda amesema tangu kuanza kwa mradi mwaka
2021, wataalamu walibainisha baadhi ya maeneo yaliyopo ndani ya halmashauri zinazotekeleza
mradi ili kuonesha juhudi na hatua mahsusi zinazochukuliwa na Serikali kwa
kushirikiana na wadau katika urejeshaji wa uoto wa asili.
“Moja ya eneo ambalo tunaweza kujivunia kwa sasa katika
mradi ni urejeshaji wa uoto wa asili…kati ya vijiji 54 vya mradi tuna vijiji
ambavyo kwa sasa suala la uoto wa asili limeleta manufaa manufaa makubwa ya
kijamii na kiuchumi” amesema Dkt. Mapunda.
Ameongeza kuwa kupitia mpango wa urejeshaji, baadhi ya
maeneo yaliyopewa kipaumbele ni pamoja na uhifadhi wa vyanzo
vya maji, huduma za mifumo ikolojia pamoja na shughuli za kilimo
mseto.
Aidha Dkt. Mapunda amesema kupitia uhifadhi misitu
jamii, mradi umewezesha shughuli endelevu na wezeshi ikiwemo kilimo, uvuvi na
ufugaji wa kisasa na kusaidia uhifadhi wa mazingira na kufanya usimamizi wa rasilimali zilizopo na kuandaa mpango matumizi bora ya ardhi.
Kwa mujibu wa Dkt. Mapunda amesema Serikali kupitia Ofisi
ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imepanga kuhakikisha
Tanzania inafikia malengo ya kidunia ya kurejesha ekari Milioni 2.5 za uoto wa
asili nchini ifikapo mwaka 2030.
Kuhusu vipaumbele vya bajeti ya mradi kwa mwaka 2024,
Dkt. Mapunda amesema jumla ya vipaumbele vitano vimeainishwa kwa ajili ya utekelezaji
wa shughuli mbalimbali za mradi ambapo moja ya kipuambele hicho ni usimamizi wa
biashara ya kaboni.
Ametaja vipaumbele vingine ni kuwezesha wakulima
kutekeleza shughuli za miradi ya mabadiliko ya tabianchi, ufugaji endelevu,
kuhamasisha shughuli mbadala za kiuchumi pamoja na uboreshaji wa miundombinu ya
shughuli za uzalishaji mali.
Kwa upande wake Mshauri wa Kiufundi kutoka Shirika la
Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira (IUCN), Doyi Mazenzele amesema Shirika hilo
kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais imeendelea kuweka mikakati ya
pamoja kwa kuendelea kuhimiza jamii kutambua umuhimu wa utunzaji wa bioanuai ambazo
zinachangia upatikanaji wa huduma ikolojia.
“Tumeendelea kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais
pamoja na Wizara mbalimbali katika kuwajengea uwezo wa kitaalamu wananchi na
wasimamizi wa miradi katika maeneo ya halmashaur” amesema Mazenzele.
Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya
Iringa, Bw. Robert Masunya amesema Halmashauri hiyo imeendelea na juhudi
mbalimbali za uhifadhi wa mazingira na urejeshaji wa uoto wa asili kwa kuhimiza
shughuli wezeshi zisizoharibu mazingira ikiwemo matumizi ya nishati safi ya
kupikia.
“Tumeendelea kuhakikisha shughuli za uhifadhi zinapewa
kipaumbele katika maeneo yote ndani ya Halmashauri ambayo yanatekeleza mradi
kwa ikiwemo ulinzi wa vyanzo vya maji kwa kuhamasisha wananchi kutunza maeneo
hayo" amesema Masunya.
Mradi wa SLR unafadhiliwa na Mfuko wa Mazingira wa
Dunia (GEF) kupitia Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) na kusimamiwa na Ofisi ya Makamu
wa Rais ambapo kiasi cha Bilioni 25.8 kimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa
mradi huo.
Mradi huo ulioanza mwaka 2021 unatarajia kukamilika mwaka 2025 na kunufaisha jumla ya Mikoa 5,
Halmashauri 7, Kata 18 na vijiji 54. Halmashauri zinazonufaika na mradi ni
Iringa Vijijini, Mbeya, Mbarali, Sumbawanga vijijini, Tanganyika na Mpimbwe.
MWISHO
Post a Comment