MWANAMKE ALIA MIMBA ZAKE KUPOTEA MAZINGIRA TATA

 

*******

Na Daniel Limbe,Chato

 MWANAMKE mmoja mkazi wa kijiji cha kitela wilayani Chato mkoani Geita,aliyejulikana kwa jina la  Kephren Thomas( 26) ameiomba jamii imsaidie kutatua tatizo kupotea kwa mimba zake katika mazingira ya kutatanisha,huku daktari bingwa wa magonjwa ya wanawake akizungumzia hali hiyo.

Mwanamke huyo mwenye mtoto mmoja wa kiume(9), akizungumza na vyombo vya habari ameeleza kusikitishwa kwake na hali ya kubeba ujauzito na baada ya miezi kadhaa hali hiyo hutoweka na kurejea kwenye mzunguko wake wa hedhi.

"Nimefikisha mimba mbili zinapotea,yakwamza ilikuwa mwaka 2022 nilibeba na nikaanza kuhudhuria kliniki kama kawaida nikiwa na dalili zote za ujauzito lakini baada ya miezi sita mimba yangu ilipotea na nikarudi kwenye mzunguko wangu wa hedhi kama kawaida".

"Mimba ya pili nilibeba mwaka jana 2023 nilikwenda hospitali ya wilaya ya Chato na kuanza kuhudhuria kliniki na vipimo vikionyesha nina mimba,lakini baada ya miezi minne baadaye mimba ilipotea katia mazingira ya kutatanisha".

Anasema mpaka sasa bado hajaelewa kinachosababisha hali hiyo huku akiiomba jamii kumsaidia kuondoa Changamoto hiyo kwa sababu anatamani kupata mtoto mwingine lakini mimba zake zimakuwa zikipotea.

"Nashukuru mme wangu bado hajaonyesha kuninyanyapaa kutokana na hali hiyo,ila nafsi yangu inaumia sana kwa hali inayonitokea bora hata mimba zingekuwa zinatoka nikaona hata damu kuliko kupotea tu kisha tumbo linarejea kama zamani na kuendelea na mzunguko wangu wa hedhi"amesema Kephren.

Hata hivyo anaeleza kuwa ameshindwa kwenda kwenye uchunguzi wa vipimo vikubwa vya kimaabara kutokana na umaskini wa kipato unaomkabili na kwamba yupo tayali kufanya uchunguzi wa kina iwapo atapata wasamalia wema wa kumgharamia vipimo na matibabu.

Baadhi ya majirani zake ambao hawakutaka kutajwa majina yao, wamelihusisha suala hilo na imani za kishirikina kwa madai kuwa siyo jambo la kawaida mimba kupotea badala ya kutoka katika njia za kawaida.

"Hapa hata ukubali au ukatae lazima kuna mkono wa mtu, huyu dada zimefika mimba mbili zinapotea sisi ni mashuhuda kabisa wa hali hiyo,amekuwa anabeba na tumbo linakuwa kubwa tu lakini baada ya muda mnashangaa hana tena ujauzito kama mnaweza kumpatia mganga wa kienyeji anaweza kumsaidia kwenye tatizo hili".

"Hata sisi ni wanawake ambao tumezaa na tuna watoto,ipo hali ya mimba kutoka ambalo ni jambo la kawaida ila siyo suala la mimba kupotea tu, hapa kuna mambo ya jadi anafanyiwa huyu dada pasipo yeye kujua"amesema mmoja wa majirani zake.

 KAULI YA DAKTARI BINGWA 

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake kutoka Hospitali ya rufaa ya kanda Chato,Dkt. Osward Lyapa, amesema hakuna utafiti wa kitaalamu unaothibitisha kuwa mimba inaweza kupotea katika mazingira ya kutatanisha.

Aidha anakiri kuwepo kwa baadhi ya wanawake wenye kudai kuwa ni wajawazito lakini baada ya uchunguzi wa kimaabara huthibitika kutokuwa na hali hiyo.

Dkt. Lyapa anaeleza kuwa malalamiko mengi ya namna hiyo yanatokana na sababu mbali mbali ikiwemo changamoto ya afya ya akili,kansa na wengine kutumia njia kama hizo kunusuru ndoa zao.

"Zipo sababu mbalimbali zinazoweza kumfanya mwanamke kuamini kuwa ana ujauzito wakati siyo kweli, kwanza kuna hali ya kutamani sana kubeba mimba,hali ambayo hutokana na suala zima la kisaikolojia ambapo mtu huamini kuwa ni mjamzito na dalili zote za ujauzito huonekana ikiwa ni pamoja na kutoona hedhi,tumbo kujaa,kichefuchefu na hata matiti kuanza kujaa".

"Wengine hutokana na aina frani ya saratani (kansa) ambapo tumboni huonekana ni mjamzito hata baadhi ya kemikali zinazozalishwa kwenye mimba zinaonekana kwenye vipimo na unaweza kuamini ni mjamzito na kumruhusu kuanza mahudhurio ya kliniki kutokana na dalili zote za mimba kuwepo nazo".amesema Dkt. Lyapa

Aidha amesema ipo pia hali ya wauguzi kuamini historia waliyopewa na mhusika pasipo kujiridhisha katika vipimo vya kisayansi ambapo humuanzishia mahudhurio ya kliniki na baadaye kugundua kuwa mlengwa hana ujauzito kama ilivyo kusudiwa.

Mbali na hali hiyo pia ipo aina nyingine ya watu kusingizia hali hiyo ili kunusuru mahusiano ya kindoa na wengine kunusuru unyanyapaa wanaotendewa na mama na dada za mume.


Dkt. Bingwa wa Magonjwa ya wanawake,Osward Lyapa, kutoka Hospitali ya rufaa Kanda Chato.
******

 MATIBU YA HALI HIYO 

Dkt. Lyapa anasema wanawake wengi wenye hali hiyo,hupatiwa matibabu mbalimbali ikiwemo ya kisaikolojia ambapo baada ya kuthibitika kwenye vipimo hupewa ushauri nasihi na kurejea kwenye hali zao za kawaida.

"Wengi wao huthibitika kuwa na tatizo la kisaikolojia kutokana na matamanio makubwa ya kubeba ujauzito, ambapo hujikuta wakiamini kuwa wana mimba kisha dalili zote za mjamzito huonekana na pale tunapoubaini ukweli huwa tunawapa ushauri nasaha na baadhi yao baada ya muda mfupi huanza kuona hedhi zao zinarejea kama kawaida japo wapo ambao huendelea na hali hiyo kwa muda mrefu kidogo"amesema

Hata hivyo amesema mbali na msaada wa kisaikolojia baaadhi ya watu hao hutakiwa kupata huduma za karibu ili kuwaondolea changamoto ya afya ya akili kwa lengo la kuwarejesha kwenye hali ya kawaida badala ya kuwa na matumaini hewa.

Vilevile Dkt. Lyapa anawashauri wauguzi kutumia taaluma yao kuwapokea na kuwahudumia walengwa kupitia njia ya kisayansi badala ya kuamini tu maelezo ya wahusika kisha kuwaanzishia mahudhurio ya kliniki hali inayoweza kumsaidia mhusika mapema kuliko mtu kuchukua muda mrefu akiamini ni mjamzito wakati siyo kweli.

                           Mwisho.

0/Post a Comment/Comments