RAIS SAMIA APEWA KONGOLE KWA JESHI LA UHIFADHI

.............

Na Sixmund Begashe - Serengeti

Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya uongozi wa Mhe. Waziri, Angellah Kairuki, imempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kulijengea uwezo kiutendaji Jeshi la Uhifadhi, kutekeleza majukumu yake ya kuhifadhi na kulinda Maliasili za nchi kwa manufaa ya kizazi kilichopo na kijacho.

Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anaeshughulikia Maliasili, Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba, alipokuwa akifunga mafunzo ya awali ya Jeshi la Uhifadhi, katika Kambi ya Fort Ikoma Wilaya ya Serengeti Mkoa wa Mara kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii.

CP. Wakulyamba amebainisha kuwa Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi mahiri wa Mhe. Rais Samia imeendelea kutoa ajira kwa askari wapya na vitendea kazi ikiwemo magari, mitambo, vifaa vya mawasiliano na vifaa vingine vya kupambana na changamoto ya Wanyamapori wakali na waharibifu pamoja na wahalifu (majangili).

"Kwa niamba ya Waziri wa Maliasili na Utalii na Wizara kwa ujumla, nipende kumuahaidi Mhe. Rais kuwa Jeshi letu la Uhifadhi litaendelea kutekeleza majukumu yake kwa weledi na nidhamu ya hali ya juu ili kuunga mkono juhudi zake katika uhifadhi wa maliasili zetu kwani sote tunatambua kuwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ndiye mhifadhi namba moja". Alisema CP. Wakulyamba.

Licha ya kuwapongeza kwa kufanikiwa kupata mafunzo yaliyowajengea uwezo wa usimamizi wa rasilimali za Wanyamapori na Misitu ndani na nje ya maeneo yaliyohifadhiwa CP. Wakulyamba amewahasa wahitimu hao, kuyaishi kwa vitendo mafunzo hayo katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku kwenye vituo vyao vipya vya kazi.

"Ni tegemeo langu pia kuwa mafunzo haya yamewajengea uzalendo, uadilifu, ujasiri, utayari, kujiamini pamoja na kuwapa mbinu na ari kubwa katika kulinda Maliasili za Taifa". Alisisitiza CP. Wakulyamba.

Naye Naibu Kamishna wa Uhifadhi na Maendeleo Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) Massana Gibrill Mwishawa amefafanua kuwa kwa miezi Sita kambini hapo, askari hao wamejifunza nadharia na vitendo ikihusisha matumizi sahihi ya silaha, ulengaji shabaha, mbinu mbalimbali za kupambana na uhalifu, huduma ya kwanza, uzalendo, uadilifu, ukakamavu, sheria mbalimbali zinazosimamia maliasili, haki za binadamu, ukamataji wa wahalifu na uendeshaji wa kesi mahakamani.

Mafunzo ya awali ya ajira mpya (“WFCS Recruit Course”) kwa Askari Uhifadhi – TANAPA 217 yalijumuisha mafunzo ya mabadiliko ya utendaji kazi kutoka mfumo wa kiraia kuingia mfumo wa Kijeshi/Jeshi la Uhifadhi Wanyamapori na Misitu (“WFCS Transformation Course”) kwa Maafisa Uhifadhi 07 na Askari Uhifadhi 06.

 

0/Post a Comment/Comments