*****
Tausi Mbowe, Iringa
Tatizo la bidhaa duni na bandia ni janga linaloikumba dunia. Tatizo hilo pia limejipenyeza nchini ambako wafanyabiashara wasio waaminifu wamekuwa wakitengeneza bidhaa mbalimbali ikiwano dawa na vifaa tiba visivyo na viwango.
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Peter Serukamba ametoa onyo kali kwa wafanyabiashara wanaowauzia wananchi kinyemela dawa duni na bandia.
Serukamba ametoa tahadhari hiyo katika kikao kazi cha baina ya Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba Tanzania (TMDA) na Wahariri na Waandishi wa habari kutoka mikoa ya Iringa, Dodoma na Singida.
Kikao hiko cha siku mbili kimefanyika mkoani Iringa, Mei 16, 2024.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa huyo, waandishi wa habari wanapaswa kuzingatia maaadili ya uandishi wa habari ili kuepuka upotoshaji na taharuki kwa jamii.
AlisemaTMDA haiwezi kutekeleza majukumu yake bila ushirikiano kutoka kwa waandishi wa habari kwa andika habari zenye tija.
'Mkifanya kazi kwa kushirikiana na jamii mtafahamu changamoto zinazowakabili wanachi katika masuala yanayohusu ubora na usalama wa dawa na vifaa tiba, 'alisisitiza Serukamba.
Serukamba alisema waandishi wa habari wanaumuhimu mkubwa wa kuwa makini katika kubaini bidhaa duni na bandia ili kuwaokoa wananchi na athari zinazoweza kupatikana na matumizi yake.
Aidha, Mkuu huyo wa mkoa aliipongeza TMDA kwa kazi nzuri inayoifanya hasa ya kutoa elimu kwa wananchi juu ya madhara ya bidhaa duni na bandia.
Awali Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Dk Adam Fimbo alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya mamlaka hiyo na vyombo vya habari katika utoaji wa elimu ya afya kwa wananchi juu ya matumizi wa bidhaa za dawa na vifaa tiba.
Alisema wanahabari wanapaswa kuungana na mamlaka hiyo ili kuunganisha nguvu kwa pamoja juu ya ufuatiliaji wa bidhaa duni na bandia nchini.
"Pamoja na mafaniko mengi tuliyoyapata katika mamlaka yetu bila kuhusisha wanahabari lengo letu la kulinda afya za wananachi halitofikiwa ndiyo maana mara kwa mara tunashirikiana nao. "
Katika kikao hicho mada mbalimbali ziliwasilishwa kwa washiriki zikihusu kazi za TMDA ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa sheria na masuala yanayohusiana na udhibiti wa bidhaa za dawa na vifaa tiba..


Post a Comment