SERIKALI IMEJIPANGA KUENDELEA KUHUDUMIA WANANCHI


....................
Na: Issah Mohamed - Dar es Salaam

EMAIL:issahmohamedtz@gmail.com

Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imesema itaendelea kuwahudumia wananchi na kuhakikisha wanapata huduma bora na kwa wakati unaotakiwa kwa lengo la kuwaletea maendeleo na Taifa kwa ujumla.

Kauli hiyo imetolewa  na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu, Jenista Mhagama wakati alipotembelea banda jumuishi la Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizopo chini yake katika maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (SABASABA) ili kujionea jinsi watumishi wa ofisi hiyo wanavyotoa huduma kwa wananchi na wadau kwa ujumla.

Bi Mhagama amepongeza huduma zinazoendelea kutolewa pamoja na elimu juu ya shughuli zinazotekelezwa na ofisi yake huku akiwasihi watumishi wa ofisi hiyo kuzingatia weledi, ufanisi, huduma nzuri na kuzingatia misingi ya utumishi wa umma wawapo katika utekelezaji wa majukumu hayo.

“Tuendelee kuwahudumia wananchi, na tumeamua kuwafikia kwa karibu kupitia maonesho haya hivyo tunawakaribisha wananchi wote kuendelea kutembelea banda la Ofisi ya Waziri Mkuu, tumejiandaa vizuri kuwa hudumia,” amesema Waziri Mhagama.

Aidha ametumia nafasi hiyo kueleza juhudi za Serikali kwa kuendelea kuimarisha diplomasia na kuimarisha sekta zote nchini katika kuhakikisha nchi inajipatia maendeleo zaidi.

Maonesho hayo ya 48 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanaongozwa na kauli mbiu isemayo “Tanzania: Mahali Sahihi Pa Biashara na Uwekezaji,”.

0/Post a Comment/Comments