_*Na Mwandishi wetu;-*_
Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Daniel Sillo (Mb) ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani nchini, ameongoza Kikao cha Dharura *Na.1/2024* cha Baraza hilo kilichofanyika leo Julai 18, 2024 katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi Ndogo za Wizara hiyo Jijini Dar es Salaam.
Kikao hicho kimejadili agenda mbalimbali ikiwemo Mikakati na Maandalizi katika kuelekea Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani kwa Mwaka 2024 na Miaka 50 ya Baraza hilo ambayo Kitaifa yanatarajiwa kufanyika Mkoani Dodoma.
Awali akisoma taarifa yake Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani ambaye ni Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Kamishna Msaidizi wa Polisi Ramadhan Ng’anzi ameeleza kuwa Hali ya Usalama Barabarani nchini imeendelea kuimarika kutokana na utekelezaji wa Operesheni za ukamataji wa makosa hatarishi, Utoaji wa elimu, Ukaguzi wa magari na usimamizi wa watendaji wa Kikosi cha Usalama barabarani.
Aidha Wajumbe wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani walipata fursa ya kutoa maoni yao mbalimbali kuhusu agenda zilizojadiliwa katika Kikao hicho sambamba na kutoa ushauri wa nini kifanyike katika kuelekea Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani kwa Mwaka 2024 na Miaka 50 ya Baraza hilo.
Post a Comment