Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu
wa Rais Bi. Chrstina Mndeme (kulia) akiwa katika picha ya pamoja na Naibu
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) Bi.
Elizabeth Mrema mara baada ya kikao cha pembeni wakati wa Mkutano wa Wawakilishi
wa Kudumu wa UNEP
*********
Tanzania imeahidiwa na Shirika la Mazingira la
Umoja wa Mataifa (UNEP) kuungwa mkono katika vipaumbele vya mazingira ikiwemo agenda
ya nishati safi ya kupikia.
Hayo yamejiri wakati wa mazungumzo kati ya Naibu
Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme amekutana
na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa UNEP Bi. Elizabeth Mrema Julai 11, 2024 jijini
Nairobi, Kenya.
Mazungumzo hayo yamefanyika katika kikao cha
pembeni baina ya viongozi hao wakati wa Mkutano wa 11 wa Wawakilishi wa Kudumu
wa UNEP uliotarajiwa kumalizika Julai 12, 2024.
Bi. Mndeme ameishukuru UNEP kwa kuisaidia
Tanzania katika utekelezaji wa miradi mbalimbali yenye lengo la kuhifadhi
mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Halikadhalika, ameliomba shirika hilo kuendelea
kuunga mkono Tanzania hususan katika utekelezaji wa vipaumbele vya nchi katika
sekta ya mazingira vikiwemo agenda ya nishati safi ya kupikia, biashara ya
kaboni na uchumi wa buluu.
Bi. Mrema ameishukuru Serikali ya Tanzania
kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa michango yake kwenye agenda zilizowasilishwa
na kujadiliwa kwa kipindi chote cha mkutano huo.
Kutokana na hatua hiyo Naibu Mkurugenzi huyo
amepokea michango hiyo na kuahidi kuichukua kwa ajili ya kuweka kwenye vipaumbele
kwenye mpango kazi wa Shirika la UNEP katika kipindi cha mwaka 2024-2025 kwa
ajili ya kuifanyia kazi.
Mkutano wa 11 wa Wawakilishi wa Kudumu wa UNEP
unafanyika kwa lengo la kupitia programu za shirika hilo UNEP kwa kipindi cha
mwaka 2022- 2023 na kupitia mpango kazi na bajeti kwa mwaka 2023 – 2024.
Pia, katika mkutano huo wajumbe wanapitia utekezaji wa kazi za
shirika hilo hususan kwenye masuala ya mabadiliko ya tabianchi, bioanuwai na
uchafuzi wa mazingira.
Sanjari na hayo, pia wajumbe wa mkutano huo uliofunguliwa Julai
08, 2024 wamepata wasaa wa kufanya maandalizi ya mikutano ijayo ya Baraza la
Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEA - 7).
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo umewakilishwa na Naibu
Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais Bi. Christina Mndeme na Balozi
wa Tanzania nchini Kenya Mhe. Dkt. Bernad Kibesse.
Post a Comment