ACT WAZALENDO KUSIMAMISHA WAGOMBEA KATIKA MITAA, VIJIJI NA VITONGOJI VYOTE NCHINI


 *******

Jana, tarehe 25 Agosti, 2024 Halmashauri Kuu ya Chama cha ACT Wazalendo chini ya Mwenyekiti wake Ndg. Othman Masoud Othman imekutana katika kikao chake cha kawaida katika ukumbi wa Hakainde Hichilema uliopo Jengo la Maalim Seif, Makao Makuu ya Chama, Magomeni Dar es salaam.

Pamoja na mambo mengine, Halmashauri Kuu imepokea na kujadili  taarifa mbalimbali na kuzitolea maamuzi na maagizo kama ifuatavyo:-

a) Uteuzi wa Nafasi MbalimbaliHalmashauri Kuu ya Chama kwa madaraka yake iliyonayo kwa mujibu wa Katiba ya Chama imethibitisha uteuzi wa nafasi mbalimbali kama ifuatavyo:-

) Imethibitisha uteuzi wa Ndg. Ester Akoth Thomas kuwa Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara. Kabla ya uteuzi huo, Ndugu Ester Akoth Thomas alikuwa Naibu Katibu wa Idara ya Oganaizesheni, Mafunzo na Uchaguzi Taifa. 

ii) Imethibitisha uteuzi wa Ndg. Omar Ali Shehe kuwa Naibu Katibu Mkuu Zanzibar. Kabla ya uteuzi huo, Ndg. Omar Ali Shehe alikuwa Katibu wa Oganaizesheni, Mafunzo na Wanachama. 

iii) Imethibitisha uteuzi wa Ndg. Shaweji Mketo kuwa Naibu Katibu wa Oganaizesheni, Mafunzo na Wanachama kuziba nafasi ya Ndg. Ester Akoth Thomas ambaye ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Tanzania Bara. Kabla ya uteuzi huo, Ndg. Shaweji Mketo alikuwa Katibu wa Idara ya Haki za Binadamu na Vyombo vya Uwakilishi wa Wananchi. 

iv) Imethibitisha uteuzi wa Ndg. Savelina Mwijage kuwa Naibu Katibu wa Ngome ya Wanawake Taifa.

v) Imethibitisha uteuzi wa Ndg. Mbarala Maharagande kuwa Katibu wa Idara ya Haki za Binadamu na Vyombo vya Uwakilishi wa Wananchi. 

vi) Imethibitisha uteuzi wa Ndg. Khamis Ali Salum kuwa Naibu Katibu wa Idara ya Oganaizesheni, Mafunzo na Uchaguzi. 

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Chama Taifa kwa madaraka yake aliyonayo kwa mujibu wa Katiba ya Chama amemteua Makamu Mwenyekiti Bara Ndg. Isihaka Rashid Mchinjita kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Maadili Taifa. Wajumbe wa Kamati ya Maadili walioteuliwa na kuthibitishwa na Halmashauri Kuu ni hawa wafuatao:-

-Adv. Moza Mohamed Khamis, 

-Adv. Emmanuel Mvula

b) Maandalizi ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa Mwaka 2024

Halmashauri Kuu ya Chama imepokea na kujadili taarifa ya maandalizi ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2024. Halmashauri Kuu imeazimia Chama kusimamisha wagombea kwenye Mitaa, Vijiji, na Vitongoji vyote nchini. Halmashauri Kuu ya ACT Wazalendo imeielekeza Sekretarieti ya Chama kutumia mtandao wetu mpana wa wanachama kuhakikisha tunasimamisha wagombea ngazi zote za Serikali za Mitaa bila kuacha hata Kitongoji, Kijiji na Mtaa.

c) Programu ya Mikutano ya Hadhara

Halmashauri Kuu imepokea na kujadili taarifa ya programu za Chama za hamasa na ujenzi wa Chama zilizofanyika Tanzania Bara na Zanzibar. Kwa upande wa Tanzania Bara programu ya mikutano ya hadhara inayoitwa "Miezi 10 Wanachama Milini 10" imefanyika kwenye mikoa 22 na jumla ya majimbo 125. Kwa upande wa Zanzibar programu imefanyika katika mikoa 10 ya Kichama.

Halmashauri Kuu imeagiza Programu ya Bandika Bandua, ya Mikutano ya Hadhara kwa kila wiki kwa upande wa Zanzibar iendelee.

Kwa upande wa Bara Halmashauri Kuu imeagiza utekelezaji wa Awamu ya pili ya ziara ya Miezi 10 Wanachama Milioni 10 utekelezwe kwenye Mikoa na Majimbo yote ambayo hayakupitiwa katika awamu ya kwanza. Ziara hiyo inatarajiwa kuanza tarehe 10 Septemba 2024. 

d) Kugawanywa kwa Mkoa wa Pwani

Halmashauri Kuu imeridhia mapendekezo ya kuugawa mkoa wa Pwani na kupatikana mikoa miwili ili kuleta ufanisi wa kiutendaji. Mikoa miwili iliyopatikana kutokana na hatua hiyo ni mkoa wa Mwambao utakaokuwa na majimbo ya Rufiji, Mafia, Kibiti na Mkuranga. Na mkoa wa Pwani utakaokuwa na majimbo ya Kisarawe, Kibaha Vijijini, Kibaha Mjini, Chalinze na Bagamoyo.

Katika hatua nyingine, Halmashauri Kuu imeagiza kufanyika kwa uchambuzi wa kina wa mikoa yenye sifa na vigezo vya kugawanywa ili kukidhi malengo ya ufanisi wa kiutendaji na ya kimkakati ya Chama.

Imetolewa na:

Shangwe Ayo

Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma.

0/Post a Comment/Comments