********
Chama Cha Wandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kimewapiga msasa Wahariri wa vyombo mbalimbali vya Habari nchini juu ya umuhimu wa uhifadhi na mazingira.
Mafunzo hayo pia yalikuwa na lengo la kuwapa uelewa Wahariri katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na umhimu wa ushirikishwaji wa sekta binafsi katika shughuli za uhifadhi.
Akizungumza katika mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kupitia Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, Meneja wa Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi, Mradi wa USAID Tuhifadhi Maliasili, Dk. Elikana Kalumanga amesema kuwa kama sekta binafsi itashirikishwa kikamilifu inaweza kuendelea kuwa na mchango mkubwa zaidi katika pato la Taifa.
”Ipo haja ya ushirikishwaji wa sekta binafsi katika kukabiliana na changamoto zilizopo kwenye shoroba za wanyamapori.
“Shughuli za kibimadamu zimekuwa zikifanyika kwenye shoroba hivyo tunahitaji ushiriki wa pamoja katika kulinda na kuhifadhi viumbe hai nchini,” amesema Dk. Kalumanga.
Ameeleza kuwa katika uhifadhi zipo fursa nyingi ambazo Watanzania wakizitumia vizuri hasa katika sekta ya utalii ni fursa kubwa kwao kujiongezea kipato.
“Katika kazi hizi za uhifadhi zipo fursa nyingi,mojawapo ni ya kutumia utalii ambapo uwekezaji wake ni rahisi, ambapo unaweza kuweka matenti na vyoo vya kuhamisha, na watalii wakafurahia na kupata fedha “alisema Dk. Kalumanga.
Ameongeza kuwa kuna umuhimu wa jamii hasa zile zilizopo katika maeneo yenye kupakana na hifafhi kuzipata fursa hizo ikiwemo kufanya kilimo cha viungo na mbogamboga ambacho hustawi zaidi katika maeneo ya hifadhi.
Dk. Kalumanga alibainisha kuwa kilimo cha viungo na mbogamboga ni biashara yenye tija na faida kwa jamii kwani hata katika mradi huo umekuwa ukisaidia jamii kujiendeleza katika kilimo hicho.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa JET, Dkt. Ellen Otaru akifungua semina hiyo, amesema lengo la kukutana na Wahariri ni kupanua wigo wa ufahamu kuhusu uandishi wa taarifa za uhifadhi na mazingira ili kuleta matokeo chanya kwa jamii.
Post a Comment