*******
Na Daniel Limbe,Chato
KITENDO cha shirika la umeme nchini(Tanesco) kukata ovyo umeme pasipo taarifa rasmi kwa jamii kimeonekana kuwakera madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Chato mkoani Geita ambapo wamemtaka meneja wa shirika hilo wilayani humo kujitathimini.
Hatua hiyo imetajwa kurudisha nyuma maendeleo ya wananchi kutokana na shughuli za kiuchumi kukwama na wengine kuharibika vifaa vyao baada ya umeme kukatika na kuwaka ghafra.
Mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Christian Manunga,amesema hayo kwenye kikao cha robo ya nne ya baraza la madiwani hao ambalo pia limesisitiza kuongezwa kasi ya ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuiwezesha halmashauri hiyo kujiendesha.
"Kitendo cha kukatika ovyo umeme kinatuumiza sana,tena umeme unakatwa hadi usiku na kusababisha matukio ya wizi kuongezeka kwa wananchi wetu,ninataka Tanesco watueleze sababu ni nini" amesema Manunga.
Kadhalika amesema ili miradi ya wananchi iweze kukamilika kwa wakati ipo haja kwa watumishi wa halmashauri hiyo kuweka mkazo kwenye ukusanyaji wa mapato ya ndani badala ya kusubiri pesa kutoka serikali kuu.
Mkurugenzi wa halmashauri hiyo,Mandia Kihiyo,ametumia fursa hiyo kutangaza rasmi msimu mpya wa kilimo 2024/25 ambao unalenga kuihamasisha jamii kuzalisha mazao ya kilimo na biashara kwa tija ili wananchi waweze kujikwamua kiuchumi.
Amesema hali ya chakula ni nzuri kwa wananchi wa wilaya hiyo kutokana na mafanikio makubwa ya kilimo kwa msimu wa mwaka 2023/24 ambapo baadhi ya wananchi wamenufaika ki uchumi na kubaki na ziada ya chakula.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Chato,Christian Manunga,akitoa msimamo wa Baraza hilo juu ya kukatika ovyo umeme.
Post a Comment