KUKIUKWA MWONGOZO WA AFYA CHANZO CHA WATUMISHI WASIO NA UBORA*

Wanachuo wakiendelea kusherehekea mahafali yao
.....................

Na Daniel Limbe,Chato

KUKIUKWA kwa mwongozo wa Wizara ya Afya kuhusu gharama za mafunzo kwa vitendo kwa wanafunzi wa vyuo vya kati imetajwa kuwa kikwazo cha kupata wahitimu bora katika taaluma ya afya kutokana na baadhi yao kushindwa kumudu gharama hizo.

Licha ya Wizara hiyo kutoa mwongozo wa mwaka 2021 unaoainisha gharama za mafunzo ya vitendo kwenye hospitali nchini,utekelezaji wake umekuwa kizungumkuti kutokana na baadhi ya halmashauri kujipangia gharama zao kinyume na maelekezo ya serikali.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa Chuo cha sayansi za Afya na teknolojia Chato(Ccohest) Dkt. Joel Maduhu,wakati wa mahafali ya saba ya chuo hicho,ambapo ameiomba serikali kushinikiza mwongozo huo kufuatwa ili kutoa unafuu kwa wanafunzi wa taaluma ya afya nchini.

"Tumekuwa tukisumbuliwa kwa wanafunzi kutakiwa kulipia kiasi kikubwa cha fedha kwa kila mwanafunzi anapokuwa kwenye mafunzo ya vitendo(field attachment) kwa maelezo kuwa Baraza la madiwani limepitisha gharama hizo ambazo ni kinyume na mwongozo wa wizara ya elimu" anasema Dkt. Maduhu. 

Kwa mujibu wa mwongozo huo,wanafunzi kuanzia 1 hadi 25 wanapaswa kulipia kiasi cha sh. 250,000 kwa kipindi cha mwaka mmoja huku wanafunzi 25 hadi 50 wanapaswa kulipia sh. 500,000.

Kadhalika wanafunzi kuanzia 50 hadi 75 hupaswa kulipa sh. 750,000 na kuanzia 75 hadi 100 wanapaswa kulipa Sh. 1,000,000 na kwamba wanafunzi 100 na kuendelea wanapaswa kulipia sh. 1,5000,000 kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Kutokana na hali hiyo,Dkt. Maduhu anasema ipo haja kwa serikali kutoa maelekezo maalumu kwa wakurugenzi wa halmashauri za wilaya ili kuheshimu mwongozo wa serikali na kwamba ikiwezekana gharama hizo ziondolewe kabisa.

Baadhi ya wahitimu wa kada za afya kwenye chuo hicho,Winfrida Vicent na Joseph Nyakuya,wamesema gharama hizo zimekuwa kikwazo kikubwa kwa baadhi ya wanafunzi hao kutokana na baadhi yao kutoka familia duni na masikini zaidi.

Hata hivyo wameiomba serikali kuongeza bajeti ya Wizara ya afya ili kuajili watumishi wengi wa kada hiyo hasa kwenye zahanati na vituo vya afya kwa madai ndiko kuna wananchi wengi wanaopoteza maisha kwa kukosa huduma bora.

"Tunaiomba serikali yetu itoe kipaumbele cha ajira za kada ya afya kwa sababu wananchi hasa walioko vijijini wanapoteza maisha kutokana na kukosa huduma bora zilizo karibu yao,ikizingatiwa huduma zinazotolewa ngazi ya mikoa na Kanda ni ghari ukilinganisha na uwezo wa wananchi wenyewe" amesema Winfrida.

0/Post a Comment/Comments