Na Daniel Limbe,Karagwe
KUTOKANA na ongezeko la uharibifu wa mazingira unaosababishwa na shughuli za kibinadamu nchini,shirika lisilo la kiserikali la "Mavuno project"wilayani Karagwe mkoani Kagera limeanzisha kilimo rafiki wa mazingira ili kunusuru nchi kuwa jangwa siku za usoni.
Mbali na hilo, kilimo hicho kimesaidia kuongezeka kwa chakula, kuinua uchumi pamoja na kupambana na changamoto ya utapiamlo kwa watoto.
Akizungumza na mwandishi wetu kuelekea maadhimisho ya miaka 30 ya shirika hilo,Mtaalamu wa kilimo na mazingira, Kilamba Clodwig,amesema kilimo hicho ni rafiki wa mazingira na mavuno yake ni makubwa na yenye uhakika.
Zaidi ya wakulima 55,935 wamenufaika na miradi huo katika wilaya ya Karagwe na Kyerwa,na kwamba tathmini iliyofanywa na asasi hiyo imeonyesha mafanikio makubwa kutokana na wananchi kuinua uchumi wa familia zao ukilinganisha na awali kabla mradi huo haujaanza kutekelezwa.
Baadhi ya wananchi walionufaika na mradi huo wilayani Karagwe,mbali na kulishukuru shirika la Mavuno,
wamesema kilimo hicho kimesaidia kupunguza hali ya utapiamlo kwa watoto wao baada ya kuwa na uhakika wa chakula.
"Zamani tulikuwa tukiamini kilimo cha kutawanya mazao ndiyo chenye kumpatia faida mkulima kumbe sivyo,kwa sasa tunalima eneo dogo lakini mavuno yake ni makubwa na yenye uhakika"amesema Gresiana Method.
"Kilimo tunachofanya hakina gharama kubwa isipokuwa unapaswa kutunza hali ya udogo kwa kuweka mbolea asilia aina ya samadi, kuchagua mbegu nzuri ya kupanda,ikiwa ni pamoja na kuweka mazao yanye jamii tofauti ili kuweka ukinzani wa magonjwa ya mimea"amesema.
Kutokana na hali hiyo Mkurugenzi wa shirika hilo,Charles Bahati,akasema anajivunia asasi hiyo kutimiza miaka 30 ya uwepo wake kwa jamii sambamba na wananchi kuendelea kuunga mkono jitihada za shirika hilo hasa katika uhifadhi wa mazingira na uhakika wa chakula.
"Lengo letu kuu ni kuhakikisha tunaimalisha uwezo wa jamii katika kutambua raslimali walizonazo, kuzisimamia na kuziendeleza kwa maendeleo endelevu na kwamba nguvu yetu kubwa tumeielekeza kwenye kata 30 "amesema Bahati.
Kadhalika ametumia fursa hiyo kuipongeza halmashauri ya wilaya ya Karagwe na Kyerwa kwa ushirikiano mkubwa wanaoutoa kwa taasisi hiyo na kwamba imekuwa ni rahisi kwao kutimiza malengo yao ya kuihudumia jamii kwa mafanikio makubwa zaidi.
Hata hivyo amesema ajenda ya utunzaji wa mazingira na kilimo endelevu ni muhimu sana kwa jamii kutokana na ukweli kwamba jamii yenye chakula cha kutosha inauwezo wa kufanya kazi na kuinua uchumi wa kaya na taifa kwa ujumla.
Vilevile utunzaji wa mazingira ni njia bora ya kumheshimu Mwenyezi Mungu kwa kuwa ndiye mwanzilishi wake,na ameagiza kupitia kitabu kitakatifu cha Biblia
Mwisho.
Post a Comment