MWANARIADHA WA TANZANIA ATWAA TUZO YA KIMATAIFA CRDB MARATHON-BURUNDI*.

Kushoto ni mwanariadha,Imelda Mfungo,katikati na kaimu Meneja CRDB tawi la Chato na wa mwisho kulia ni Katibu tawala wilaya ya Chato,Thomas Dimme,akipokea bendera ya taifa kutoka kwa mwanariadha wa Tanzania.
 ...................

Na Daniel Limbe, Geita

MWANARIADHA kutoka Tanzania,Imelda Mfungo,amefanikiwa kuipeperusha vyema bendera ya nchi baada ya kuibuka mshindi wa tatu katika mashindano ya kimataifa ya CRDB Marathon yaliyofanyika nchini Burundi.

Zaidi ya wanariadha 400 wameshiriki mbio hizo kutoka mataifa mbalimbali ambapo washindi wametunukiwa fedha na medali.

Mashindano hayo yamehusisha mbio za km 10 ambapo mshinda wa kwanza ametoka nchini Burundi, wapili kutoka nchini Algeria kisha namba tatu ikatwaliwa na mwakilishi pekee kutoka Tanzania.

Aidha mashindano hayo yamekusanya zaidi ya wanariadha 1,000 ambao wameshiriki katika mbio tofauti huku wakimbiaji 400 wakishiriki kwenye mbio za km 10.

Baada ya ushindi huo Imelda ameishukuru halmashauri ya wilaya ya Chato mkoani Geita kwa kumuandaa vyema katika mashindano mbalimbali ya riadha ndani na nje ya nchi na kwamba matamanio yake ni kuiwakilisha nchi katika mashindano makubwa ya Olimpiki.

Hata hivyo mwanariadha huyo amesema anamshukuru mwenyezi Mungu kwa kufanikiwa kutwaa tuzo hiyo kwa sababu ni heshima kwake na taifa kwa ujumla.

Kadhalika ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuandaa mashindano hayo huku akipendekeza awamu ijayo kufanya uratibu mzuri wa mbio hizo ikiwa ni pamoja na kuwatenganisha wakimbiaji wa kike na kiume kuliko ilivyofanyika mwaka huu kwa kuwaunganisha jinsia zote kukimbia kwa wakati mmoja.

Ofisa Michezo wilaya ya Chato,Abel Mataba,amesema mashindano ya "CRDB International Marathon" yamesaidia kuitangaza nchi kimataifa na kwamba ipo haja kubwa kwa serikali kuboresha miundo mbinu ya michezo ili kuibua vipaji vingi kwa jamii.

Kaimu meneja wa CRDB tawi la Chato,Mbaruku Salum,amempongeza mwanariadha huyo kwa kuitetea vyema bendera ya taifa na kwamba uongozi wa tawi hilo utaandaa zawadi maalumu kwaajili ya kumkabidhi mshindi huyo nje ya tuzo aliyopokea nchini Burundi.

Akipokea bendera ya taifa kutoka kwa mwanariadha huyo kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Chato, Katibu tawala wa wilaya hiyo Thomas Dimme,mbali na kumpongeza kwa ushindi huo amemtaka mwanariadha huyo kuendelea kuitetea wilaya ya Chato,katika mashindano mbalimbali ili kuitangaza ndani na nje ya nchi.

"Tunakupongeza sana kwa kutuheshimisha kama wilaya ya Chato,mkoa wa Geita na taifa kwa ujumla,ushindi ilioupata ni sifa kwetu watanzania,tunaamini utaendelea kuwa balozi mzuri wa vivutio vya utalii vilivyopo kwenye wilaya yetu ikiwemo hifadhi ya taifa ya kisiwa cha Rubondo na hifadhi ya taifa ya Burigi-Chato".

"Kutokana na heshima hiyo kubwa kwa Tanzania,ninakuahidi kukupatia kiasi cha shilingi 200,000 mwishoni mwa mwezi huu, na hiyo ni zawadi yangu binafsi kutokana na furaha niyoipata" amesema Dimme.

Kadhalika kupitia Ofisi ya mkuu wa wilaya hiyo, ameahidi kumpatia hati ya pongezi baada ya taratibu za kiutumishi kukamilika ili iwe kumbukumbu kwa kazi nzuri aliyoifanya katika mashindano yao ya kimataifa

0/Post a Comment/Comments