********
Na Mwandishi Wetu
Wakala wa Usalama na Afya
Mahali pa Kazi (OSHA) umeelezea umuhimu wa kulinda uwekezaji mkubwa uliofanywa
na serikali katika rasilimali watu kuanzia wanapozaliwa hadi kufikia hatua ya kuajiriwa
au kujiajiri katika shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Umuhimu huo umeelezwa na
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, alipokuwa akiwasilisha mada kuhusu
masuala ya Usalama na Afya kazini katika semina ya waajiri na viongozi wa
matawi ya Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya Tanzania (TUGHE) inayofanyika
Jijini Arusha kuanzia Agosti 26 hadi 29, 2024.
Kiongozi
huyo Mkuu wa Taasisi ya OSHA amesema hadi kufikia hatua ya mtu kuwa na ujuzi
fulani na kuajiriwa ama kujiajiri, serikali inakuwa imewekeza kwa kiwango
kikubwa ikiwemo kugharamia huduma za afya tangu utotoni pamoja na kumpatia
elimu ya kumwezesha kupambana na mazingira yake.
“Serikali
yetu inawekeza fedha nyingi katika kuwahudumia watu wake tangu akina mama
wanapokuwa wajawazito, wanapojifungua na kulea watoto wao ikiwemo kuwapatia
elimu katika ngazi tofauti,” ameeleza Mtendaji Mkuu wa OSHA na kuongeza:
“Kwa
mantiki hiyo serikali inategemea kupata faida ya uwekezaji uliofanyika kwa watu
wake (return on investment) kupitia watu hao kushiriki katika shughuli
mbalimbali za kiuchumi kwa kipindi kirefu. Jambo ambalo litawezekana tu endapo
wafanyakazi katika sehemu za kazi watalindwa dhidi ya vihatarishi vya magonjwa,
ajali na vifo vinavyoweza kutokea katika sehemu za kazi.”
Hivyo,
Mtendaji Mkuu wa OSHA ametoa wito kwa waajiri na wafanyakazi kuhakikisha kwamba
katika sehemu zao za kazi kunakuwa na mifumo madhubuti ya usalama na afya ikiwa
ni pamoja na kuzingatia taratibu zote muhimu za usalama na afya kama
inavyoelekezwa na wataalam kutoka katika Ofisi yake.
Kwa
upande wake, Mwenyekiti wa TUGHE, Bw. Joel Kaminyoge, ameeleza jinsi
wanavyoshirikiana na OSHA katika kutoa elimu ya masuala ya usalama na afya kwa
waajiri na wafanyakazi nchini hususan wanachama wa TUGHE.
“OSHA ni wadau wetu wakubwa
sana ambao mbali na kufadhili shughuli zetu mbalimbali wamekuwa wakishirikiana
nasi katika kutoa elimu ya usalama na afya kwa wanachama wetu katika mikutano
yetu kama huu unaoendelea hapa Jijini Arusha,” ameeleza Comred Kaminyoge.
Akielezea umuhimu wa semina
mbalimbali wanazofanya kwa waajiri na viongozi wa matawi ya TUGHE, Bw.
Kaminyoge, amesema semina hizo zimesaidia kwa kiwango kikubwa kuboresha maslahi
ya wafanyakazi pamoja na kupunguza migogoro mahali pa kazi.
OSHA ni Taasisi chini ya Ofisi
ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) iliyokabidhiwa wajibu wa
kusimamia utekelezaji wa Sheria Na. 5 ya Afya na Usalama Mahali pa Kazi ya
mwaka 2003 pamoja na kanuni zake. Kupitia sheria hiyo maeneo yote ya kazi
nchini yanapaswa kusajiliwa na OSHA na kuingizwa katika utaratibu wa ukaguzi wa
mifumo ya usalama na afya unaofanywa na OSHA kila mwaka.
Mtendaji Mkuu wa OSHA, Khadija Mwenda, akiwasilisha mada kwenye semina ya waajiri na viongozi wa matawi ya Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE) inayofanyika Jijini Arusha Agosti 26 hadi 29, 2024.
Baadhi ya watumishi wa OSHA pamoja na washiriki wengine wakifuatilia matukio mbalimbali katika semina ya waajiri na viongozi wa matawi ya Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE).
Washiriki wa semina ya waajiri na viongozi wa matawi ya Chama cha Wafanyakazi wa Serikali na Afya (TUGHE), wakifuatilia mada mbalimbali katika semina hiyo inayofanyika Jijini Arusha Agosti 26 hadi 29, 2024.
Post a Comment