Jeshi la Polisi Kamisheni ya Zanzibar limetoa onyo kwa watu wanaosambaza taarifa za kutekwa kwa watoto visiwani humo.
Aidha, Jeshi hilo linamshikilia Habibu Rashid Omar (35), mkazi wa Mwera kwa tuhuma za kuchapisha taarifa ya uongo kupitia mitandao ya kijamii kuhusiana na kutekwa kwa watoto wanne katika Skuli ya Regezamwendo hali iliyosababisha taharuki kwa jamii.
Naibu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Naibu Kamishna wa Polisi DCP, Zuberi Chembera amesema Zanzibar ni salama na hakuna tukio lolote la utekwaji wa watoto na kuwataka wananchi kupuuza taarifa za upotoshaji zinazosambazwa kupitia mitandao ya kijamii.
“Niwahakikishie kwamba Zanzibar ni salama, watoto wetu wako salama, wanakwenda shule nakurudi nyumbani salama, wazazi tuendelee kuwaangalia watoto wetu, tuendelee kuwatunza watoto wetu kwa maadili mema kama tuna shaka ya jambo lolote tulitolee taarifa kwenye vyombo vya usalama vinavohusika badala ya kuandika kwenye mitandao ya kijamii ambayo mwisho wake inasababisha taharuki” alisisitiza Chembera.
DCP Chembera alisema Jeshi la Polisi linaendelea kufanya uchunguzi na kuwafikisha mahakamani watuhumiwa wote watakaobainika kuhusika na usambazaji wa taarifa za uzushi.



Post a Comment