********
Naibu Waziri Nishati, Judith
Kapinga amesema Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan amejidhatiti vyema
katika kusambaza miradi ya umeme mijini na vijijini na sasa umekuwa si anasa
tena kutokana na wananchi kuutumia kwa
shughuli za kiuchumi na kijamii.
Kapinga ameyasema hayo leo
Agosti 16, 2024 wakati akizindua huduma ya umeme katika Kijiji cha Mpingi
Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.
"Ni dhamira ya Mhe.
Rais kuhakikisha Vijiji vyote 12,318 nchini vinapata umeme, kupitia Wakala wa
Nishati Vijijini (REA), tumebakisha chini ya Vijiji 151 kuvipelekea umeme na
kazi inaendelea." Amesema Mhe. Kapinga
Kapinga ameongeza kuwa
Serikali inakwenda kufuta historia ya Vijiji vya Tanzania kutokuwa na umeme
kutokana na Vijiji vyote kwenda kufikiwa na nishati hiyo.
Aidha, kutokana na kuelekea
kukamilika kwa upelekaji wa umeme kwenye Vijiji, Kapinga amesema sasa Serikali
imeelekeza nguvu katika usambazaji wa umeme kwenye Vitongoji.
Amewahakikishia Watanzania
kuwa, Serikali itaendelea kupeleka huduma ya umeme katika maeneo yote nchini
ili watanzania waweze kuboresha shughuli za kiuchumi.
Awali, Robert Dulle ambaye
ni Msimamizi wa miradi ya umeme vijijini Mkoa wa Ruvuma alitoa wito kwa
wananchi kuchangamkia fursa ya uwepo wa umeme kwa kuunganisha kwa gharama ya
shilingi 27,000 tu.
Post a Comment