.......................
๐ *Lengo ni kuimarisha upatikanaji umeme katika maeneo yote nchini
๐ Mradi kugharimu shilingi Trilioni 4.42
๐ Vituo nane vyakamilika; sita vipo asilimia 97
Naibu Waziri Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt. Samia Suluhu Hassan ameridhia Wiizara ya Nishati kupitia TANESCO kujenga vituo 75 vya kupokea, kupoza na kusambaza umeme ikiwa ni jitihada zake za kuhakikisha wananchi katika maeneo yote wanapata umeme wa uhakika.
Mhe. Kapinga amesema hayo Agosti 04, 2024 wakati wa ziara ya Rais, Mhe. Dkt. Samia katika kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Ifakara mkoani Morogoro.
"Kabla ya mwaka 2021 nchi ilikuwa ina vituo 61 tu vya kupokea na kupoza umeme, tunakushukuru sana Mhe. Rais kwa kuridhia ujenzi wa vituo vingine vipya 75." Amesema Mhe. Kapinga
Kapinga ameeleza kuwa, ujenzi wa vituo hivyo vipya utagharimu takribani shilingi Trilioni 4.42 ambapo mradi huo unatekelezwa kwa awamu.
Ameongeza kuwa, katika mradi huo tayari vituo nane vimejengwa na kuanza kazi huku vituo sita vikifikia asilimia 97.
Akizungumzia ujenzi wa kituo cha kupoza umeme cha Ifakara, Kapinga amesema kuwa, kimeleta tija kwani kwa kukamilika kwake licha ya kupeleka umeme wa uhakika kwa wananchi, kimewezesha takribani viwanda vipya 54 kuunganishwa na huduma ya umeme.
Akizungumzia kuhusu miradi ya kuiunganisha Tanzania na Nchi za Ukanda wa Mashariki mwa Afrika na Nchi za Ukanda wa Kusini mwa Afrika, amesema Rais Samia amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha Tanzania inaungana na nchi hizo kupitia miradi mbalimbali kama wa TAZA.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mha. Hassan Saidy amesema kituo cha Ifakara kimejengwa kutokana na uhitaji mkubwa wa umeme wilayani Ifakara, Malinyi na Ulanga na hii pia inatokana na shughuli kubwa za kilimo na uchimbaji madini.
Mha. Hassan ameongeza kuwa, kabla ya ujenzi kituo cha Ifakara umeme kwa mwezi ulikuwa ukikatika mara 18 ambapo hivi sasa ikitokea umeme umekatika basi ni mara moja.
Post a Comment