.......,...................
📌 *Asema Serikali itaendelea kupeleka umeme maeneo ya uwekezaji*
📌 *Serikali kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji*
Naibu Waziri Nishati, Mhe. Judith Kapinga amesema Serikali imetenga takribani shilingi bilioni 4.6 kupeleka umeme kwenye maeneo ya migodi mkoani Ruvuma.
Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Agosti 18, 2024 wakati akizindua Kituo cha Mauzo ya Makaa ya Mawe ya kampuni ya Market Insight Limited (MILCOAL), inayojihusisha na uchimbaji, uuzaji na usambazaji wa Makaa ya Mawe, Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.
"Hapa katika mgodi wa MILCOAL tutatumia takribani shilingi milioni 280 kuleta umeme, nguzo tayari zimeshawekwa na sasa hivi wataalam wameanza kazi ya kuvuta waya." Amesema Mhe. Kapinga
Ameongeza kuwa, Serikali kupitia Wizara ya Nishati inatekeleza miradi ya kupeleka nishati ya umeme kwenye maeneo makubwa ya uwekezaji ikiwemo migodini.
Mhe. Kapinga amesisitiza kuwa makaa ya mawe ni chanzo cha nishati thabiti na ya kutegemewa katika maeneo ya uwekezaji mkubwa hususani viwandani.
Amewapongeza MILCOAL kwa uwekezaji huo ambao unachangia ukuaji wa uchumi wa nchi.
Amewahakikishia wawekezaji kuwa, Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji ikiwemo ujenzi wa miundombinu wezeshi na kuongeza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inathamini wawekezaji.
Post a Comment