TANI 61,000 ZA MBOLEA YA NPK KUONGEZA UZALISHAJI WA TUMBAKU KWA MSIMU WA KILIMO 2024/2025

.....................

Kampuni ya  Mbolea Tanzania (TFC) na Kiwanda cha Mbolea cha United Capital Fertilizer Zambia Company Limited (UCFL) zimesaini mkataba wa uagizaji wa mbolea tani 61,000 ya NPK kwa ajili ya kilimo cha tumbaku kwa msimu wa kilimo 2024/2025.

Mkataba huo umesainiwa leo tarehe 23 Agosti, 2024 na Mkurugenzi Mkuu wa TFC, Bw. Samwel Mshote na Mtendaji Mkuu wa UCFL, Bw. Huang Yaochi na kushuhudiwa na Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb); Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo (Ushirika na Umwagiliaji), Dkt. Suleiman Serera; Mkurugenzi Mtendaji Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Bw. Joel Laurent; Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Tumbaku, Bw. Stanley Mnozya, Viongozi na Watumishi wa Wizara ya Kilimo.

Makubaliano hayo yamelenga kuongeza tija na uzalishaji wa zao la tumbaku nchini kwa kuhakikisha kuwa kuna upatikanaji wa mbolea ya uhakika kwa wakulima ambapo kwa mujibu wa taarifa aliyoitoa Mkurugenzj Mkuu wa TFC Mshote ni kwamba mbolea hizo zitaanza kuingia nchini kuanzia tarehe 26 Agosti 2024.

Uagizaji wa Mbolea hizi umekidhi viwango vinavyohitajika katika kilimo cha Tumbaku nchini Tanzania na umezingatia vigezo vilivyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Nchini (TFRA).

0/Post a Comment/Comments