Wageni mbalimbali wakiwa katika picha ya pamoja kwenye kituo cha Afya Kamuli wilayani Kyerwa mkoani Kagera.
Mganga mfawidhi wa kituo cha Afya Kamuli,Ramadhan Mrisho,akitoa maelezo mbalimbali ya utoaji huduma za afya.
Mwonekano wa vipande vya ufuaji wa umeme jua(Solar) kwenye kituo cha afya Kamuli wilayani Kyerwa.
.........................
Na Daniel Limbe,Karagwe
IMEELEZWA kuwa upatikanaji wa umeme wa jua (Solar) kwenye baadhi ya vituo vya afya wilayani Kyerwa mkoani Kagera umesaidia kunusuru afya za wajawazito na watoto kutokana na kuimarika kwa matibabu ikiwemo upasuaji.
Kadhalika imesaidia kupunguza gharama za uendeshaji wa vituo hivyo baada ya kushuka kwa gharama za malipo ya umeme wa Tanesco.
Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kyerwa, Dk. Shafi Mziray, amesema hayo baada ya kutembelewa na wageni kutoka shirika lisilo la kiserikali la Mavuno Project lililopo wilayani Karagwe ambao ni wafadhili wa umeme jua kwenye vituo vya afya, zahanati,shule za msingi na sekondari.
Pia ziara hiyo iliwashirikisha wahisani mbalimbali kutoka nchini,Ujerumani,
Swiden na Austria ambao ni miongoni mwa wafadhili wa shirika la Mavuno ambalo linatekeleza miradi mbalimbali ya jamii kwenye wilaya ya Karagwe na Kyerwa mkoani Kagera ikiwemo usambazaji wa umeme jua kwenye taasisi binafsi na umma.
Mganga mfawidhi wa kituo cha afya Kamuli,Dkt. Ramadhan Mrisho, amesema awali matumizi ya umeme kwa mwezi mmoja ilikuwa ikiwagharimu kati ya shilingi 500,000 hadi 550,000 na baada ya kupata ufadhilii wa umeme jua gharama zimeshuka kufikia shilingi 200,000 hadi 250,000.
"Tunashukuru sana shirika la Mavuno kwa kutufungia umeme jua maana imetusaidia sana kupunguza gharama za kulipia umeme wa Tanesco,pia imeongeza ufanisi wa kazi kutokana na huduma za upasuaji wa kawaida kufanyia hapa hapa badala ya kwenda hospitali ya wilaya"amesema Mrisho.
"Mpaka muda huu mmenikuta hapa natoka kufanya upasuaji kwa mjamzito,lakini yote haya yanafanyika kutokana na uwepo wa uhakika wa umeme, kwa kuwa hata umeme wa Tanesco,unapokosekana haituzuii kuwahudumia wateja wetu kwa maana umeme wa jua upo wakati wote".
Hata hivyo amesema baadhi ya wagonjwa ambao hupewa rufani ya kwenda hospitali ya wilaya hiyo hulazimika kusafiri umbali wa zaidi ya km 20 na baadhi yao kutumia gharama kubwa kwenda hospitali ya Nkwenda ili kupata huduma za upasuaji mkubwa.
Mtaalamu wa umeme jua(Solar) kutoka shirika la Mavuno,Edwin Mugarula, amesema waliguswa na afya za jamii hasa iliyopo vijijini kutokana na baadhi ya vituo vya afya kutokuwa na uhakika wa nishati ya umeme,hivyo kusababisha baadhi ya huduma muhimu za afya kukosekana kwa wakati.
Amesema shirika hilo limefanikiwa kutoa msaada wa umeme jua kwenye vituo vya afya vitano vilivyopo wilayani Kyerwa na Zahanati mbili zilizopo kwenye wilaya ya Karagwe kwa lengo la kuhakikisha jamii iliyopo vijijini inanufaika na huduma za afya kama ilivyo kwa waliopo mijini.
Kutembelewa kwa miradi mbalimbali inayotekelezwa na shirika la Mavuno project inalenga kuona ufanisi wa huduma kwa jamii ikiwa ni kuelekea maadhimisho ya miaka 30 ya utendaji kazi wa shirika hilo tangu kuanzishwa kwake mwaka 1993.
Mwisho
Post a Comment