WATAKAO SHINDWA KUWASILISHA VIELELEZO KWA CAG KUKIONA CHA MOTO B'MULO


 Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo,Leo Rushahu,akitoa msimamo wa Baraza hilo.

********

Na Daniel Limbe,Biharamulo

BARAZA la madiwani wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera limetishia kuwachukulia hatua kali baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo watakaoshindwa kuwasilisha vielelezo vya ukaguzi hesabu kwa Mkaguzi na mdhibiti mkuu wa hesabu za serikali(CAG).

Uamuzi huo umetolewa na mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo,Leo Rushahu,wakati akifafanua siri ya kuvuka malengo ya ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri hiyo kwa kipindi cha mwaka 2023/24.

Akiwa katika kikao cha kujadili na kupitisha taarifa ya hesabu za mwisho wa mwaka wa bajeti ya 2023/24,Rushahu ametumia fursa hiyo kumpongeza mkurugenzi wa halmashauri hiyo,Innocent Mukandala, pamoja wa watumishi wengine kwa kazi kubwa ya kukusanya na kusimamia mapato ya halmashauri hiyo.

Pongezi hizo zimetolewa baada ya mweka hazina wa halmashauri hiyo kuwasilisha taarifa ya makadirio ya mapato na matumizi ya halmashauri hiyo kwa mwaka wa fedha uliomalizika na kuonyesha mafanikio makubwa kwa kuvuka lengo kusudiwa.

Aidha amesema mafanikio ya hesabu hizo lazima yaakisi uhalisia kwenye ukaguzi wa CAG ikiwa ni pamoja na kuwasilisha nyaraka zote muhimu zitakazohitajika wakati wa ukaguzi huo ili kuondoa hoja zisizokuwa za lazima.

Kwa mujibu wa mweka hazina wa halmashauri hiyo,Stella Gibson, takribani shilingi bilioni 45.5 zimekusanywa katika bajeti ya mwaka 2023/24 ambayo ni sawa na aslimia 111 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 41.077.

Kadhalika jumla ya shilingi Bilioni 41.4 zimetumika kwa matumizi mbalimbali na kuifanya halmashauri hiyo kuwa na uwezo mkubwa wa kuendesha baadhi ya miradi yake pasipo kutegemea serikali kuu.

Kutokana na hali hiyo,Diwani wa kata ya Runazi,Aniceth Bruno,na diwani wa kata ya Kalenge,Erick Method, wamepongeza hali hiyo na kudai imesaidia kutatua baadhi ya changamoto mbalimbali ya miradi ya maendeleo iliyokuwa imekwama kwa bajeti ya mwaka 2022/23.

Kadhalika wamesema mafanikio hayo yanatokana na ushirikiano mkubwa kati ya madiwani na wataalamu wa halmashauri hiyo ikiwa ni pamoja na kubuni na kuanzisha vyanzo vipya vya mapato ya ndani,kusimamia na kutumia fedha kwa nidhamu.

Baadhi ya madiwani wakiendelea kujadili hoja ya mapato na matumizi ya fedha za halmashauri hiyo.

Mweka hazina wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo,Stella Gibson,akiwasilisha kwenye kikao cha madiwani taarifa ya mapato na matumizi ya fedha za halmashauri hiyo.
Mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Biharamulo,Leo Rushahu,akitoa msimamo wa Baraza hilo.

                       Mwisho.

0/Post a Comment/Comments