CP. WAKULYAMBA ATOA SOMO

..................

Na Sixmund Begashe - Morogoro

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii anaeshughulikia Maliasili Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba amekutana na Menejimenti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) ambapo pamoja na mambo mengine amezungumza na Maofisa na Askari wa Taasisi hiyo kwa lengo la kupata uwelewa wa pamoja juu ya uboreshaji wa shughuli za TAWA kwa kuzingatia maelekezo au maoni ya Tume ya Haki Jinai.

CP. Wakulyamba ameutaka uongozi wa Mamlaka hiyo kuendelea kusimamia vyema taratibu na kanuni za Jeshi la Uhifadhi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa kiwizara na kitaifa kwa ujumla na kuonya kuwa atakaeenda kinyume cha sheria, atachukuliwa hatua za kinidhamu na ikibidi hatua za kisheria.

Akizungumza na Askari hao baada ya mafunzo yaliyotolewa na Maafisa wa Jeshi la Polisi kutoka Makao Makuu Dodoma, CP. Wakulyamba licha ya kuwapongeza kwa kazi nzuri wanazofanya amewasisitiza askari hao kuendelea kufanya kazi kwa weledi na uwadilifu mkubwa wanapotekeleza majukumu yao na kuhakikisha wanaendelea kupambana na changamoto ya Wanyamapori wakali na waharibifu katika makazi ya wananchi.

Aidha, kwa upande mwingine maafisa kutoka Jeshi la Polisi; Joseph Jingu na Oscar Felician walioambatana na Kamishna Wakulyamba walisisitiza utunzaji na matumizi sahihi ya silaha kwa mujibu wa sheria za nchi. Waliwakumbusha Askari madhara yanayoweza kuwapata kutokana na matumizi yasiyo sahihi ya silaha za moto

Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi, Kaimu Naibu Kamishna wa Uhifadhi TAWA, Mlage Kabange alimshukuru Kamishna Wakulyamba kwa ziara yake na kuahidi kuzingatia na kutekeleza maelekezo yote yaliyotolewa

Ziara hiyo ya CP. Wakulyamba imelenga kuimarisha Utendaji kazi wa Taasisi zinazounda Jeshi la Uhifadhi kwenye nyanja ya Uhifadhi wa Maliasili nchini kupitia mafunzo maalumu kwa ushirikiano na Jeshi la Polisi Tanzania.


 

0/Post a Comment/Comments