"MASONYA IMEBEBA HISTORIA ADHIMU" DKT. NTANDU

   .........................

Na Sixmund Begashe - Tunduru

Mkurugenzi wa Idara ya Mambo ya Kale Dkt. Christowaja Ntandu akiwa ameambatana na Mkurugenzi Msaidizi, Maendeleo Malikale na Makumbusho Bw. William Mwita, amefika Shule ya Sekondari ya Wasichana Masonya kwa lengo la kujionea hali ya uhifadhi wa eneo hilo la kihistoria lililotumiwa na wanawake kutoka nchi ya Msumbiji kama kambi wakati wa kupigania uhuru wa nchi yao kuanzia mwaka 1966 Hadi 1975

Akizungumza na Uongozi wa Shule hiyo yenye historia adhimu, Dkt. Ntandu amesema Wizara kupitia Idara anayoiongoza itaendelea kushirikiana na wananchi pamoja na wadau wa uhifadhi kuhakikisha maeneo yote ya kihistoria nchini ikiwemo Shule hiyo ya Sekondari Masonya, yanahifadhiwa na kutangazwa kama sehemu ya kuchechemua utalii nchini.

Dkt. Ntandu ameongeza kuwa, Tanzania imejaliwa kuwa na utajiri mkubwa wa urithi wa malikale, hivyo ni vyema wananchi wote wayalinde maeneo hayo ili kizazi kijacho kije kufaidi utajiri huo wa kipekee unaopatikana hapa nchini pekee.

"Eneo hili ni miongoni ushahidi wa mchango wa Tanzania katika upatikanaji wa uhuru wa nchi za Kusini mwa Bara la Afrika". Alisema Dkt. Ntandu

Aidha Dkt. Ntandu ametoa wito kwa watanzania kujitokeza kwa wingi kutumia maeneo hayo kwa faida za kijamii na kiuchumi nchini, huku akitaja fursa katika sekta hiyo ni pamoja na kukarabati majengo na kuhuisha matumizi yake, kuanzisha makumbusho, kuandaa makala simulizi na kuanzisha matamasha ya kumbukumbu nk.

Naye Mwalimu Mkuu Msaidizi wa Shule hiyo ya Masonya iliyopo Tunduru Mkoa wa Ruvuma, Mwl. Essau Mbugi, ameipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa jitihada inazofanya katika kuhifadhi maeneo yenye historia ya Tanzania, na kuahidi kuwa uongozi wa shule hiyo utaendelea kushirikiana na Wizara katika uhifadhi wa Historia ya kambi hiyo ambayo kwa sasa ni Shule ya Sekondari ya Wasichana Masonya.

Kwa sasa Shule hiyo inahudumia wanafunzi wa kike kama sehemu ya urithi wa Kihistoria ya eneo hilo lililotumiwa kama Kambi ya kuwahifadhi wanaharakati wa Kike pamoja na Viongozi Wanawake na ndipo Umoja wa Wanawake wa Msumbiji ulipozinduliwa, pia kuna nyumba iliyotumiwa na Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere na ukumbi wa mikutano uliotumiwa na aliyekuwa Rais wa Msumbiji Samora Machel.

 

0/Post a Comment/Comments