Daniel Limbe,Biharamulo
MTOTO ambaye jina lake limehifadhiwa amenusurika kuuawa na nyani wilayani Biharamulo mkoani Kagera,baada ya wanyama hao kuvamia makazi ya wananchi na kumtwaa mtoto huyo kabla ya wananchi kumnusuru akiwa amejeruhiwa vibaya.
Diwani wa Kata ya Nyarubungo,Petro Kizuluja,ameliambia Baraza la madiwani wa halmashauri hiyo kuwa kumekuwepo na ongezeko la uvamizi wa wanyamapori kwenye makazi ya watu na kutishia uhai wa wananchi pamoja na ongezeko la utolo kwa wanafunzi.
Alikuwa akiwasilisha taarifa ya kata yake kwenye kikao cha robo ya nne katika bajeti ya mwaka 2024/25 ambapo amesema hivi sasa nyani wamekuwa tishio kubwa la uhai wa wananchi wa eneo hilo kutokana na kukaba wanawake na watoto.
Akielezea tukio la mtoto huyo,amesema mnamo Agosti 26,2024 majira ya saa 2 asubuhi mtoto huyo akiwa nyumbani kwao kwenye kijiji cha Lusabya, alitwaliwa na nyani wakati mama yake mzazi akitandaza majani kwenye shamba la migomba lililopo nyumbani hapo.
Hata hivyo baada ya kubaini kuwa mwanaye ametwaliwa na nyani, alilazimika kupiga yowe ili kuomba msaada wa jamii ambapo wananchi waliojitokeza eneo hilo walipambana na wanyama hao na kufanikiwa kumnusuru mtoto huyo licha ya kujeruhiwa maeneo ya kichwa.
Kutokana na hali hiyo ameiomba serikali kuwadhibiti wanyama waharibifu wakiwemo nyani ambao wamekuwa wakitoroka ndani ya hifadhi ya taifa ya Burigi-Chato na kuingia kwenye makazi ya watu.
Hata hivyo baadhi ya madiwani wa halmashauri hiyo,wamesema suala la nyani hao halipaswi kufumbiwa macho kutokana na madhara ambayo wamekuwa wakisababisha kwenye baadhi ya vijiji vilivyo karibu na hifadhi hiyo.
Madhara mengine ni pamoja na kushambulia mazao ya wakulima,kula wanyama wafugwao ikiwemo kuku na bata pamoja na hofu ya kuwasababishia wananchi magonjwa yatokanayo na wanyama hao ikiwemo homa ya Mpox.
Akijibu malalamiko ya madiwani hao,Ofisa maliasili wa wilaya hiyo,Thomas Mahenge, amekiri kuwepo kwa tukio hilo na kwamba jitihada za kuwaondoa wanyama hao zinafanyikaa kwa kushirikiana na Taasisi ya utafiti wa wanyama poli (TAWIRI) ambao ndiyo wenye jukumu la kuainisha panapofaa kupelekwa wanyama hao.
Hata hivyo amesema zoezi la kuwahamisha nyani hao linahitaji muda kutokana na uwepo wa tishio la ugonjwa wa homa ya nyani(Mpox) huku akidai suala la kuwaua litategemea ushauri wa madaktari ili kuona kama halitaleta madhara kwa afya ya jamii
Post a Comment