RAIS SAMIA AZINDUA MAGHALA 28 YA KUHIFADHI CHAKULA VIJIJINI

 



RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa maghala 28 ya kuhifadhi nafaka katika eneo la ghala la Luhimba, Mkoani Ruvuma leo tarehe 24 Septemba 2024 ambayo yanaenda kuwa mkombozi kwa wakulima.

“Maghala haya 28 ni sehemu ya kwanza ya utekelezaji wa maelekezo yako Mhe. Rais ya kujenga maghala 70 vijijini ambapo yana uwezo wa kuhifadhi tani 1000 kila mojawapo, kwa jumla ya tani 28000 kwa maghala yote 28,” amesema Mhe. Hussein Bashe (Mb), Waziri wa Kilimo.

Akieleza zaidi kuhusu mikakati ya utekelezaji wa kujenga maghala vijijini, Waziri Bashe amesema kuwa maghala hayo yamejengwa katika halmashauri 4 za Wilaya ambazo ni: Songea Manispaa (ghala 1), Songea DC (maghala 11), Madaba (maghala 9) na Namtumbo (maghala 7).

“Wizara ya Kilimo kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) tayari imeanza kutumia maghala 5 kuhudumia wakulima, kati ya maghala 28; ambapo kutakuwa na maghala mengine matano yanayotarajiwa kukamilika wiki chache zijazo,” amesema Waziri Bashe.

Gharama za ujenzi wa maghala 28 ni shilingi bilioni 14.7 ambapo ni gharama ya shilingi milioni 527 kwa kila ghala.

Aidha, Waziri Bashe amemueleza Mhe. Rais Dkt. Samia kuwa NFRA pia itajenga maghala makubwa ya kısasa yenye uwezo wa kuchukua tani 5000 kila ghala. Maghala hayo yatajengwa kwenye miji ya Mikoa mitano ya uzalishaji wa mazao ambayo ni Katavi, Rukwa, Ruvuma, Songwe na Tabora.




0/Post a Comment/Comments