WAZIRI MKUU: SUALA LA MAZINGIRA LIWE AJENDA YA KITAIFA


******

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema suala la uhifadhi wa mazingira liwe ajenda ya Kitaifa na jukumu la kila mmoja kuanzia ngazi ya familia mpaka Taifa.

“Na tunapokwenda kuhifadhi mazingira lazima tuanze na ngazi ya familia na tunapopanda juu tupanue wigo hadi kwa wadau mbalimbali. Viongozi wa dini mnayo nafasi kubwa na hii lazima iwe ajenda maalum, iwe ni ofisi za umma, za binafsi au kwenye taasisi.”

Ametoa kauli hiyo leo (Jumanne, Septemba 10, 2024) wakati akifunga mkutano maalum wa viongozi na wadau wa mazingira ulioitishwa ili kujadili mwenendo wa mazingira nchini. Mkutano huo ulifanyika kwenye Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete, jijini Dodoma. 

Amesema Rais Samia Suluhu Hassan amemudu kusimamia na kutoa miongozo mahsusi ya kuhakikisha mazingira yanahifadhiwa. Leo hii, tunamuona anaendelea kulisimamia ili Taifa lifanikiwe katika uhifadhi wa mazingira kwa vizazi vya sasa na baadaye. 

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwaeleza wajumbe wa mkutano huo juu ya jitihada ambazo Rais Samia amekuwa akizichukua ili kuhakikisha suala la nishati safi linakubalika.

"Rais amekuja na dhana mpya ya kukataa kukata miti na kutuhamasisha kuhusu nishati safi ya kupikia. Rais wetu amekuwa kinara wa nishati safi hadi na mwezi Mei alienda Ufaransa kuhutubia kuhusu nishati safi na yeye akiwa ni Mwenyekiti mwenza wa mkutano huo. Hii ni fahari kwa nchi yetu," amesema.





 

0/Post a Comment/Comments