Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na
Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema Bajeti ya mwaka 2025/2026 kipaumbele
kikubwa kitakuwa ni utekelezaji wa miradi mikubwa kwa ushirikiano na Sekta
Binafsi na Umma (PPP), ili kukuza uchumi kwa kasi.
Prof. Kitila Mkumbo, amesema hayo mbele ya Kamati
ya Kudumu ya Bajeti ya Bunge ambapo amenukuu kanuni ya 113(1) na (2) ya kanuni
za kudumu za Bunge iliyochapishwa Februari 2023, ambapo mapendekezo hayo
yanawasilishwa kwa kamati ili kukusanya maoni kutoka kwa wabunge wakati wa
maandalizi.
Waziri Kitila amesema serikali imejipanga kutumia
mfumo wa PPP katika utekelezaji wa miradi mikubwa, hivyo katika bajeti ijayo
wataweka nguvu huko kibajeti.
"Katika mwaka wa fedha 2025/26 kipaumbele cha
bajeti kitaelekezwa kwenye PPP kwani ndio njia inayoweza kutekeleza miradi
mikubwa inayochochea ukuaji wa uchumi na maendeleo," amesema.
Amesema mapendekezo hayo yameweka mazingira ya
mpango wa maendeleo wa taifa, unaozingatia kuimarisha uwekezaji katika sekta
mbalimbali, kujenga uchumi imara, kuongeza uzalishaji wa viwanda na kuboresha
huduma za umma.
“Mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa taifa wa
2025/26 yanaongozwa na dira ya maendeleo ya taifa 2025, ambayo inalenga kuiweka
Tanzania kati ya nchi za kipato cha kati ifikapo mwaka 2025 na kufikia viwango
vya juu vya maendeleo ya binadamu,” amesema.
Waziri Kitila amesema mapendekezo hayo yanajikita
katika kuendeleza na kutekeleza mipango ambayo inatoa matokeo katika maeneo
matano ya kipaumbele yaliyoainishwa katika mpango wa tatu wa miaka mitano.
Prof Kitila ametaja maeneo muhimu ambayo
yatatekelezwa kwa mfumo wa PPP ni miundombinu ya usafiri na uzalishaji wa
viwanda.
Kitila amesema jumla ya miradi 17 bora imepangwa
kutekelezwa katika mwaka ujao wa fedha, huku akibainisha mafanikio kutoka kwa
mpango wa sasa wa maendeleo wa 2023/24.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Oran
Njeza ameipongeza serikali kwa kuja na mpango huo na kwamba matarajio yao ni
kuona miradi inatekelezwa kwa ufanisi.
BAJETI YA 2025/26 KIPAUMBELE MIRADI YA PPP:WAZIRI KITILA MKUMBO
**********
Post a Comment