*********
Serikali imetangaza kuanza kutumia rasmi Mfumo wa mauzo kwa njia ya Mnada wa Kieletroniki unaoendeshwa na Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), kwa zao la Korosho katika msimu wa mauzo wa mwaka huu.
Msimu wa mauzo wa zao la Korosho unatarajiwa kuanza hivi karibuni ambako korosho zote zinatarajiwa kuuzwa kwa mfumo wa TMX.
Akizungumza na wadau wa zao hilo ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake mkoani Mtwara, Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe amesema lengo la kutumia mfumo huo wa TMX ni kumlinda mkulima kwa kupokea malipo moja kwa moja kutoka kwa Vyama Vikuu vya Ushirika.
“Ni Lazima tuwe na mfumo imara wa kujua zao limezalishwa na nani, eneo gani na ubora wake ili kuendana na soko la kimataifa kwa wakulima wa korosho. Mfumo wa TMX ni suluhisho linalohitajika na tutaendelea kuboresha kadri inavyohitajika,” alisema Waziri.
Alisema TMX ni mfumo unaosimamia mnada wa kijiditali kwa lengo la kuwaongezea uhakika wa masoko, uhuru wa kuamua bei, uhakika wa malipo yao pamoja na kuchochea ushindani kwa mazao ya wakulima nchini.
Hata hivyo, Waziri Bashe amewataka wakulima kuhakikisha wanazingatia ubora wa mazao yao na kuacha ujanja ujanja ili kufungua soko imara na kuongeza bei ya mazao kwenye masoko hayo.
Kwa mujibu wa Waziri Bashe, msimu uliopita uzalishaji wa korosho umeongeza na kufikia tani 310,000 kutoka 189,000 za mwaka 2022/2023.
Awali Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho, Alfred Francis alisema kuwa mfumo wa TMX umeendelea kuboreshwa kwa kushirikiana na Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA).
“Tumepanga pia kutoa mafunzo ya mauzo ya Korosho kwa kutumia mfumo wa TMX demo ili wauzaji na wanunuzi wapate elimu kabla ya kuanza matumizi yake wakati wa msimu wa mauzo,” amesisiza.
Naye Rais wa Korosho, Yusuph Nanyila alisema korosho ni moja ya mazao ya kimkakati ambalo Serikali kupitia Rais Samia Suluhu Hassan imekuwa ikitoa pembejeo ili kusaidia uzalishaji wake.
“Kwenye maendeleo kuna changamoto lakini tamko la Rais kwamba kuwa wakulima wataanza kulipwa moja kwa moja na Vyama Vikuu vya Ushirika lilikuwa la kheri kwao,” ameongeza Nanyila.
Post a Comment