*******
Watumishi wa Vyama vya Ushirika na Taasisi za Fedha wamepewa onyo kali kuacha mara moja kuhujumu malipo ya wakulima wa Tumbaku, wakibainika hatua kali zitachukuliwa dhidi yao.
“Tunasafisha Vyama vya Ushirika. Kiongozi na Mtumishi yoyote atakayehusika kwenye ubadhirifu wa fedha za wakulima, atasimamishwa kazi mara moja,” amesema Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe wakati wa mkutano wa hadhara wa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Philip Mpango katika Uwanja wa TASAF, Wilaya ya Sikonge, mkoani Tabora tarehe 11 Oktoba 2024.
Waziri Bashe amemueleza Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Mpango kuwa wizi wa fedha zaidi ya shilingi milioni 550 umefanywa katika Chama cha Ushirika cha KISANGA ukihusisha watumishi 13 wanaotoka Tume ya Ushirika, TAMISEMI na Benki ya NMB ambapo mtumishi wa Ushirika amesimamishwa kazi.
“Nimesikitishwa na kuchukizwa na vitendo hivyo, naelekeza TAMISEMI nayo imsimamishe kazi mara moja mtumishi wao. Pia Waziri Bashe wasiliana na Meneja Mkuu wa Benki ya NMB wasimamishe kazi watumishi wao wanaohusika. Taarifa apelekewe Waziri Mkuu,” ameelekeza Makamu wa Rais Mhe. Dkt. Mpango.
Amesema Waziri Bashe kuwa hatua zilizochukuliwa na Mwendesha Mashtaka wa Serikali na TAKUKURU ni shilingi milioni 117 zilizopatikana kutoka kwa washitakiwa; ambapo shilingi milioni 437 zimezuiliwa kwenye akaunti zao; ikiwa ni pamoja na nyumba na magari yao kuzuiliwa.
Waziri Bashe pia amesema kuna kampuni ya Voedsel ambayo inadaiwa Dola za Marekani 78,000 kwa wakulima wa Chama cha Ushirika cha Mtapenda ambapo hatua zinaendelea kufuatilia ili wakulima walipwe fedha zao.
“Mhe. Makamu wa Rais tabia hizo zimepelekea kubadilisha utaratibu wa malipo kwa wakulima, ili Ushirika uwe wenye ushiriki mpana. Mwanachama halali ata kama hana hisa, ushuru wake uwe ndiyo uhalali wa uanachama wake. Tunaondoa ukiritimba wa watu kwenye Vyama,” amesema Waziri Bashe.
Wilaya ya Sikonge inazalisha vizuri mazao ya kilimo ambapo uzalishaji wa Tumbaku umeongezeka kutoka tani 10,565 mwaka 2023/24 kutoka tani 2,650 mwaka 2019/2020. Uzalishaji wa mwaka 2023/24 ni Dola za Marekani milioni 23.9.
Post a Comment