CP. WAKULYAMBA AWAPIGA MSASA ASKARI WA JU KUSINI.

**********

Na Mwandishi wetu.

Maofia na Askari wanaounda Jeshi la Uhifadhi (JU) Nyanda za Juu kusini wametakiwa kuzingatia misingi ya Sheria na Kanuni za Jeshi hilo katika utekelezaji wa majukumu yao sanjari na kuheshimu utawala wa sheria na Haki za Binadamu.

Hayo yamesemwa na Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Maliasili na Utalii, nayeshughulikia Maliasili Kamishna wa Polisi Benedict Wakulyamba akiwa kwenye ziara ya kukagua Utendaji kazi wa Askari na Watumishi wa Taasisi za TAWA, TANAPA na TFS wa Mikoa ya Rukwa, Songwe, Mbeya, Njombe na Iringa.

Kamishana Wakulyamba amesisitiza kuwa nidhamu na Uadilifu katika kutekeleza majukumu ya kila siku ndiyo msingi mkuu wa Askari wa Uhifadhi katika kutunza na kulinda rasilimali za maliasili.

Akiwa kwenye Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, alitembelea Mapori ya akiba ya Rwafi na Uwanda Mkoani Rukwa, Pori la akiba la Rukwati Piti na Mpanga Kipengele Mkoani Mbeya yanayosimiwa na TAWA.

Aidha, katika ziara hiyo Kamishna Wakulyamba alipata nafasi pia ya kuzungumza na Askari wa TFS Mkoa wa Mbeya, Askari wa mashamba ya Pori la Msitu wa Mbizi Mkoani Rukwa na Pori la Msitu wa Sao Hii Mkoani Iringa.

Maofisa na Askari hao walipata fursa ya kuelimishwa kupitia mada mbalimbali zilizojikita katika masuala ya nidhamu, uadilifu na matumizi sahihi ya silaha sanjari na Misingi ya utawala wa Sheria na Haki za binadamu.

Mafunzo haya yaliyotolewa pia na maafisa kutoka Jeshi la polisi yaligusia kanuni sahihi na salama za umiliki na utunzaji wa silaha, mambo ya kuepuka wanapokuwa na sillaha za moto na madhara yatokanayo na matumizi mabaya ya silaha.

"Sisi ni Askari wa Uhifadhi, na moja ya sifa na msingi mkuu wa Askari wa Jeshi lolote duniani ni Nidhamu na Uadilifu. Askari anapaswa kutekeleza majukumu yake kwa kushirikiana na jamii inayozunguka Hifadhi kwa kusimamia mambo makubwa mawili ambayo ni nidhamu na Uadilifu" alisisitiza Kamishna Wakulyamba.

Akihitimisha ziara yake katika Ofisi za TAWA Makao Makuu ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mkoani Iringa, Kamishna Wakulyamba aliwataka Maofisa na Askari wa Uhifadhi kujiepusha na vitendo viovu ikiwemo, rushwa, ulevi wa kupindukia, kuwabambikia watu kesi au matukio ya uhalifu ya uongo na kuepuka matumizi ya nguvu yasiyo ya lazima.

Kamishna Wakulyamba alitumia ziara hiyo kusikiliza Kero za Askari na baadhi ya wananchi ambao ni wavuvi kwenye Pori la Akiba la Uwand pamoja na kukagua ujenzi wa majengo na miundombinu mbalimbali ya Wazara hiyo.

0/Post a Comment/Comments