....................
Na Sixmund Begashe
Zoezi la kutoa elimu ya Haki Jinai kwa Askari wa Jeshi la Uhifadhi imeendelea kutolewa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi nchini na kuwafikia Maafisa na Askari wa Jeshi hilo kwenye Vituo vya Askari wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) Mkoa wa Mwanza pamoja na Vituo vya askari Lamai na Kenyangaga vinavyopatikana Hifadhi ya Taifa Serengeti Wilaya ya Tarime Mkoani Mara.
Akizungumza na Maafisa na askari hao, kwa nyakati tofauti katika Kituo cha Askari wa doria Lamai, Kenyangaga na Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi Mwanza, CP. Wakulyamba amewataka askari hao kujifunza sheria mbalimbali zinazohusu Haki Jinai si kwa kwenda chuoni tu bali hata kwa kupitia tovuti kwa kuwa taaluma hiyo inapatika huko, ili kujiimarisha kwenye kipengele cha sheria hali itakayo saidia kufanya kazi kwa kujiamini na pia kujiepusha kufanya mambo kinyume cha sheria kama vile matumizi mabaya ya silaha.
"Silaha kwa askari ni dhamana yako kwa kipindi kifupi unapokuwa zamu, hivyo unatakiwa kuwa mwangalifu sana ili isilete madhara kwa askari au kwa watu wengine" Alisisitiza CP. Wakulyamba
Aidha, CP. Wakulyamba ameongeza kuwa askari anatakiwa kutunza afya yake ya mwili na akili kwa kuachana na mambo yanayoweza kuuchosha mwili kama vile unywaji wa pombe kupita kiasi, matumizi ya madawa ya kulevya ili wawe na afya njema hasa afya ya akili.
Katika mafunzo hayo, Afisa Uhifadhi Edwin Nyerembe kutoka Kitengo cha uratibu wa Jeshi la Uhifadhi, ameeleza namna Wizara inavyo ratibu shughuli za Jeshi la Uhifadhi hususani kufuatilia nidhamu za Askari. Naye Mrakibu wa Polisi Joseph Jingu kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Kikosi cha kutuliza ghasia amefundisha juu ya umiliki salama wa silaha huku Mrakibu wa Polisi Oscar Felician akifundisha mambo muhimu ambayo askari anatakiwa kufanya na ambayo hatakiwi kufanya.
Baada ya mafunzo hayo katika Chuo cha Pasiansi yaliyohudhuriwa na Maafisa na Askari kutoka TANAPA, TAWA na TFS, CP Wakulyamba alitembelea Hifadhi ya Taifa Kisiwa cha Saanane na Ofisi za TFS Kanda ya Ziwa, kupata taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya kila siku.
Post a Comment