NAIBU Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) leo jijini Dar es Salaam, amefanya ziara katika Shirika la Mawasiliano nchini Tanzania (TTCL), kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na shirika hilo.
Akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya ziara hiyo, Naibu Waziri Mhe. Mhandisi Mahundi alisema ziara hiyo ni mwendelezo wa ziara ya kujitambulisha katika taasisi na idara zilizo chini ya wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Alisema TTCL ni Shirika kongwe la mawasiliano linalotoa huduma ndani na nje ya nchini, jambo ambalo ni lakujivunia na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kitendo chake cha kuliwezesha shirika hilo.
Alisema amevutiwa na TTCL kwa sasa kwani imeendelea kutoa huduma mbalimbali za mawasiliano ambazo zinaendana na wakati, "Kama tunavyofahamu TTCL inafanya biashara na pia inatoa huduma kwa wananchi tofauti kabisa na kampuni zingine za mawasiliano ambazo zenyewe zimejikita katika kufanya biashara kwa kiasi kikubwa," Hii unaweza kuona TTCL inaweza kutoa huduma za mawasiliano kwa wananchi hata maeneo ambayo hayana faida kibiashara kwenye huduma za mawasiliano, jambo ambalo kampuni zingine za mawasiliano haziwezi kufanya hivyo," alisema Naibu Waziri.
Awali akimkaribisha, Naibu Waziri Mhe. Mhandisi Mahundi, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania – TTCL, CPA Moremi Marwa alimweleza juu ya huduma ambazo TTCL kwa sasa inaziendesha ikiwa ni pamoja na huduma za mawasiliano kupitia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa kuwawezesha watoa huduma za mawasiliano na huduma za mawasiliano ya data, ikiwemo ya Faiba Mlangoni.
Akifafanua zaidi, alisema eneo la data TTCL imeweka mkazo katika kupeleka huduma za intaneti nyumbani na katika maofisi kwa wateja wanaoitaji huduma hiyo iliyoboreshwa zaidi.
"...Tunatoa huduma za fedha kupitia T-Pesa, kampuni yetu tanzu ya kuwezesha huduma za miamala mbalimbali ya kifedha kwa wananchi. Pia tuna huduma za Data Center ambapo tunawakaribisha wateja mbalimbali kutokea sekta binafsi na ya umma kuja kutunza taarifa zao kiusalama zaidi." alisisitiza CPA, Marwa.
Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) akiwa katika picha na menejimenti ya TTCL. |
Post a Comment