*******
Naibu Waziri Nishati, Mhe Judith
Kapinga amesema ni dhamira ya Serikali kuhakikisha kuwa wananchi wote
wanaopisha miradi ya maendeleo wanalipwa fidia
kulingana na taratibu zilizopo.
Mhe. Kapinga ameyasema hayo leo Oktoba
30, 2024 bungeni jijini Dodoma wakati
akijibu swali la Mhe. Silvestry Koka, Mbunge wa Kibaha Mjini aliyetaka kufahamu
ni lini Serikali italipa fidia kwa Wananchi na kampuni zipatazo 18 zilizopo
kwenye eneo la viwanda la Zegereni Mji wa Kibaha mkoani Pwani ambao wamepitiwa
na njia ya umeme ya kV 400.
Mhe. Kapinga ameeleza kuwa, Serikali imelipa fidia awamu ya kwanza kwa takriban shilingi bilioni
29.4 kati ya shilingi Bilioni 33 zinazotakiwa kulipwa kwa wananchi wanaopisha
mradi huo wa njia ya kusafirisha umeme msongo wa Kilovoti 400 kutoka Chalinze
hadi Mkuranga mkoani Pwani.
"Katika eneo la viwanda la
Zegereni kuna wananchi na kampuni 18 ambao wanadai fidia yenye thamani ya
Shillingi billioni 1.1. Serikali inaendelea kulipa fidia hizi kadri fedha
inavyopatikana." Amesema Mhe.
Kapinga
Akijibu swali la Mbunge wa Lupembe,
Mhe. Edwin Swalle aliyeuliza ni lini Serikali itawalipa fidia wananchi wa Kata
ya Kichiwa eneo la Idumila na eneo la Luhuji Idamba, Mhe. Kapinga amesema
wananchi hao watafanyiwa tathmini ili kuweza kulipwa fidia.
Aidha, akijibu swali la Mbunge wa
Makete, Mhe. Deo Sanga aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itawalipa fidia
wananchi wa Makete waliopisha ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wa
Rumakali, Mhe. Kapinga amesema fidia kwa
Wananchi wanaopisha mradi huo ni takriban shilingi bilioni 27 na taratibu za
kulipa fidia hiyo zinaendelea.
Aliongeza kuwa, kukamilika kwa miradi
ya Rumakali na Ruhudji kutakwenda kuzalisha takriban megawati 580 za umeme.
Akijibu swali la Mbunge wa Donge, Mhe.
Soud Mohamed Juma aliyetaka kujua mkakati wa Serikali kuimarisha upatikanaji wa
huduma ya gesi kwa matumizi ya magari na mitambo nchini, Mhe. Kapinga amesema
Serikali ilishaanza programu mbalimbali za matumizi ya gesi iliyogandamizwa
(CNG) kwenye magari.
Ameongeza kuwa, Serikali kwa
kushirikiana na sekta binafsi imefanikiwa kufungua vituo 5 vya CNG na inatarajia kufungua vituo vingine 3
ifikapo mwezi Desemba, 2024.
Aidha, jumla ya vituo 13 (vituo mama 2,
vya kuhamishika 6 na vituo vidogo 5) vinatarajiwa kufunguliwa mwaka 2025.
Kuhusu kupanua wigo wa upatikanaji wa
CNG, alisema Serikali imeshaanza kufanyia kazi suala hilo kwa baadhi ya vituo vya kuhamishika kuwekwa
mkoani Dodoma na tathmini imeshaanza kufanyika.
Amesema mikakati inaendelea ili
kuhakikisha pande zote za Muungano zinanufaika na rasilimali iliyopo.
Post a Comment