Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari,
Mhe. Maryprisca Mahundi amesema nchi inakwenda kushuhudia mageuzi makubwa ya
utunzaji wa mazingira kupitia Mkakati wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia
ambao kinara wake ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia
Suluhu Hassan.
Mhe. Mahundi ameyasema hayo Jijini Dodoma wakati akihamasisha wananchi kuachana na
matumizi ya nishati isiyo safi na kuanza kupika kisasa kupitia nishati safi ya
kupikia.
"Tunaposema tutunze mazingira, tunaweza kuona takriban
hekta 469,000 za misitu zinateketea kwa mwaka
sababu ya shughuli mbalimbali za binadamu ikiwemo matumizi ya nishati
zisizo safi za kupikia (kuni na mkaa) hivyo tunapotumia nishati safi kupikia
tunaenda kutunza mazingira yetu." Ameeleza Mhe. Mahundi
Amesema mbali ya uharibifu wa mazingira ambao umekuwa
ukitokea kutokana na matumizi ya nishati
isiyo safi lakini pia kumekuwa na athari kwa watumiaji hasa kuathirika mfumo wa
upumuaji kutokana na moshi mwingi.
Ameongeza kuwa, zaidi ya watanzania 33,000 hupoteza
maisha kila mwaka kutokana na matumizi
ya nishati isiyo safi.
Ameeleza kuwa, katika
matumizi ya nishati safi ya kupikia kama vile gesi na umeme kila aina ya
chakula kinaweza kupikwa na kutilia mkazo kuwa nishati safi ya kupikia si anasa
bali inaenda kulinda afya za watumiaji pamoja na mazingira.
Post a Comment