Na. Jeshi la Polisi, Dodoma.
Jeshi la Polisi nchini limewakumbusha Wananchi wanaomiliki silaha kinyume cha sheria kutumia kipindi hiki cha msamaha uliotangazwa na Serikali kuanzia Septemba 01, 2024 hadi Oktoba 31, 2024 kuzisalimisha kwa kuwa baada ya kipindi hicho kumalizika, masako mkali utaanza na watakabainika kuwa bado wanatumia silaha hizo kinyume cha sheria hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.
Kauli hiyo imetolewa Oktoba 4, 2024 na Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime wakati akizungumza na Waandishi wa habari Makao makuu ya Jeshi la Polisi Jijini Dodoma
Misime alisema kuwa lengo la kutangaza msamaha huo ni kuhakikisha kuwa silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria zinaondoshwa katika jamii ili zisisababishe madhara kwa raia yakiwemo vifo, majeruhi, watu kuhama makazi, njaa pamoja na uchumi kuzorota
Aidha, masharti yaliyotolewa katika tangazo hilo la msamaha ni pamoja na kipindi cha usalimishaji wa silaha zinazomilikiwa kinyume cha sheria ambacho ni kuanzia Septemba 01 hadi Oktoba 31, 2024, maeneo ya usalimishaji wa silaha hizo ambayo ni vituo vya Polisi, Ofisi za Serikali za Mitaa na katika Ofisi za Watendaji Kata/Shehia pamoja na muda wa usalimishaji wa silaha ambao ni kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa kumi jioni.
Misime alizitaja silaha zinazopaswa kusalimishwa ni pamoja na silaha ambazo hazijawahi kusajiliwa nchini na zimekuwa zikimilikiwa kinyume cha Sheria na silaha ambazo hapo awali zilikuwa zinamilikiwa kihalali lakini kwa sasa wamiliki wamefariki na ndugu wa marehemu wameendelea kuzimiliki silaha hizo kinyume cha Sheria.
“Jeshi la Polisi linawahakikishia wananchi kuwa yeyote atakayesalimisha silaha hizo ndani ya kipindi cha msamaha hatoshtakiwa na wala hakutohitajika kujua jina la atayesalimisha silaha hizo wala kujua uhalifu uliotendeka kwa tumia silaha hiyo/hizo pamoja na wahusika wake siku za nyuma kabla ya msamaha kutangazwa.” Alisema Misime
Mwaka 2023 jumla ya silaha 337 na risasi 262 zilisalimishwa kwa hiari na baada ya zoezi hilo msako ulifanyika nchi nzima na watuhumiwa 176 walikamatwa na silaha 195.
Pia walikamatwa watuhumiwa 7 ambapo wanaume walikuwa ni 6 na mwanamke mmoja ambao walikutwa wakimiliki risasi 334 kinyume cha sheria ambao walifikishwa mahakamani na baadhi walitiwa hatiani na wanatumikia kifungo gerezani na wengine kesi zao zipo katika hatua mbalimbali.
Post a Comment