Meneja wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke Mhandisi Ezekiel Mashola (wa kwanza kulia) akimkabidhi zawadi ya pongezi Mkurugenzi wa Kiwanda cha Amons Groups Ltd Bw. Ahmed Abdallah (wa kwanza kushoto) wakati walipomtembelea Ofisi kwake leo Oktoba 10, 2024, Dar es Salaam kwa ajili kutambua mchango wa ulipaji wa gharama za matumizi ya nishati ya umeme kwa wakati, katikati ni Mhasibu Mkuu wa TANESCO Mkoa wa Temeke Lucy Mwaisembe. (PICHA NA NOEL RUKANUGA)
Afisa Habari, Uhusiano na Huduma kwa Wateja TANESCO Mkoa wa Temeke Lucia Renatus akizungumza jambo leo Oktoba 10, 2024, Dar es Salaam wakati Menejimenti ya Mkoa huo walipofika kiwanda cha ALAF Ltd kwa ajili ya kutoa zawadi ya pongezi ya kutambua mchango wao wa ulipaji wa gharama za matumizi ya nishati ya umeme kwa wakati.
Picha za matukio mbalimbali yakionesha Uongozi wa TANESCO Mkoa wa Temeke wakitoa zawadi kwa wateja wakubwa wakiwemo Xinrong Plastic Waste Industry Ltd, Amons Groups Ltd, ALAF Ltd, Kamal Steel, East African Polybag, Watercom, AMIGO na Colourful, Seif Impex pamoja Kioo Limited ikiwa ni sehemu ya kutambua mchango wa kulipa gharama za matumizi ya nishati ya umeme kwa wakati.
...........
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Temeke limetambua mchango wa baadhi ya wateja ambavyo ni viwanda vinavyolipa gharama za matumizi ya nishati ya umeme kwa wakati kwa kuwapatia zawadi pamoja na vyeti vya pongezi kama sehemu ya kutambua jitihada zao ambazo zimeleta tija kwa Shirika.
Akizungumza leo Oktoba 10, 2024 jijini Dar es Salaam wakati Menejimenti ya TANESCO Mkoa wa Temeke wakiwa katika ziara ya kuwatembelea wateja waliofanya vizuri kwa ajili ya kuwapatia zawadi, Meneja wa Mkoa huo Mhandisi Ezekiel Mashola, amesema kuwa ni muhimu kutambua juhudi za wateja wanaolipa kwa wakati gharama za matumizi ya umeme.
Mhandisi Mashola amesema kuwa ulipaji wa gharama za umeme kwa wakati umesaidia kufanikisha shughuli mbalimbali za utendaji wa shirika ikiwemo utekelezaji wa maboresho ya miradi jambo ambalo limesaidia kuendelea kutoa huduma bora zaidi ya matarajio ya wateja na shirika.
“Tunaomba tuendelee kulipa gharama za matumizi ya nishati ya umeme kwa wakati, TANESCO tunaendelea kuboresha huduma zetu katika kuhakikisha umeme unapatikana muda wote pamoja na kutatua changamoto za dharula” amesema Mhandisi Mashola.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baada ya kupokea zawadi pamoja na vyeti vya pongezi, wateja hao wameushukuru uongozi wa TANESCO Mkoa wa Temeke kwa kutambua mchango wao.
Mkurugenzi wa Kiwanda Cha Amsons kinachozalisha bidhaa mbalimbali ikiwemo Camel Cement, Bw. Ahmed Abdallah, amesema kuwa wataendelea kuwa wateja waaminifu kwa kulipa gharama za matumizi ya umeme, huku akitoa wito wa kupatiwa taarifa mapema wakati inapotokea tatizo la ukataji wa umeme jambo ambalo litawasaidia kujipanga kukabiliana na dharura hiyo.
TANESCO Mkoa wa Temeke imetoa vyeti vya pongezi kwa wateja mbalimbali wakiwemo Xinrong Plastic Waste Industry Ltd, Amons Groups Ltd, ALAF Ltd, Kamal Steel, East African Polybag, Watercom, AMIGO na Colourful, Seif Impex pamoja Kioo Limited.
Post a Comment