Tanzania
na Urusi zimekamilisha mkutano wa kwanza wa tume ya pamoja ya ushirikiano wa
biashara na uchumi, ambapo pande hizo zimesaini makubaliano ya kuimarisha
ushirikiano wa kiuchumi.
Mkutano
huo umefanyika jana jijini Dar es Salaam na umejumuisha shughuli mbalimbali,
ikiwemo mkutano wa wataalamu, mkutano wa tume pamoja, na kongamano la
uwekezaji, kabla ya kutia saini makubaliano hayo na waheshimiwa mawaziri.
Katika
taarifa iliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji,
Mhe. Prof. Kitila Mkumbo (Mb), pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Kiuchumi wa
Urusi, Mhe. Maxim Reshetnikov, wameeleza kwamba nchi zao zinachukua mkondo wa
uhusiano wa biashara na uchumi. Prof. Mkumbo alisisitiza kuwa miongo sita ya
uhusiano kati ya Tanzania na Urusi imekuwa imara kisiasa na kiutamaduni,
ikileta manufaa makubwa katika nyanja za elimu, sayansi, na teknolojia.
Makubaliano
yaliyotiwa saini yanazingatia kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali,
ikiwa ni pamoja na viwanda na biashara, fedha, nishati, kilimo, elimu, sayansi
na teknolojia, uchukuzi, afya, na habari, mawasiliano na teknolojia ya habari.
Aidha, maliasili, utalii, utamaduni, na michezo ni maeneo mengine ya
ushirikiano yaliyofikiwa.
Waziri
Reshetnikov alisisitiza kuwa Urusi inaona Tanzania kama mmoja wa washirika
muhimu katika ukanda wa Afrika, na kwamba lengo lao ni kuifanya Tanzania kuwa
mshirika wa kimkakati katika masuala ya biashara na uchumi.
Mkutano
huo umehudhuriwa na wageni mbalimbali, akiwemo Waziri wa Maliasili na Utalii,
Mhe. Balozi Pindi Chana, na Naibu Waziri wa Viwanda, Mhe. Exaud Kigahe, pamoja
na Mhe. Injinia Meryprisca Mahundi. Mkutano wa wataalamu uliokuwa na wajumbe
kutoka pande zote mbili uliongozwa na Katibu Mkuu Dkt. Tausi Mbaga Kida kwa
upande wa Tanzania, na Bwa. Pavel Kalmychek, Mkurugenzi wa Idara ya Ushirikiano
wa Uwili kutoka Wizara ya Maendeleo ya Kiuchumi ya Shirikisho la Urusi.
Post a Comment