***************
Dar es salaam,
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Mohamed Mchengerwa (Mb), ameeleza kwamba takribani shilingi trilioni 1.2 zitatumika kwaajili ya kuboresha miundombinu kupitia mradi wa Uendelezaji Jiji la Dar es salaam Awamu ya Pili (DMDP Phase II) unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia mkopo wa masharti nafuu.
Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo katika viwanja vya Mwembeyanga alipokuwa akishuhudia hafla ya utiaji Saini wa mikataba ya ujenzi wa barabara katika Halmashauri 5 za Mkoa wa Dar es salaam ambapo zaidi ya Km 250 za kiwango cha lami zitajengwa, Km 90 za mifereji ya maji, vituo vya mabasi 9, masoko 18, ujenzi wa madampo 3 ya kisasa kwaajili ya kuboresha usimamizi wa taka ngumu yatajengwa.
“Mradi huu unatekelezwa kwa gharama za shilingi trilioni 1.1822 ambapo trilioni 1.03 ni mkopo kutoka benki ya Dunia na shilingi bilioni 143 ni ruzuku kutoka Serikali ya Uholanzi, pia malengo ya Serikali kupitia mradi wa DMDP awamu ya pili ni kuboresha miundombinu ya msingi katika Halmashauri zote za Mkoa wa Dar es salaam pamoja na kuzijengea uwezo wa utoaji huduma kwa wananchi kupitia utekekezaji wa miradi hii”, alisema
Aidha, Mhe. Waziri amewataka TARURA kusimamia utekelezaji wa miradi kwa ufanisi pamoja na kuwasimamia Makandarasi kama ilivyofanyika katika utekelezaji wa miradi ya DMDP awamu ya kwanza ambapo imepelekea wabia wa maendeleo (Benki ya Dunia) kutuamiini na kutupatia fedha za utekelezaji wa DMDP awamu ya pili katika Halmashauri zote tano.
Pia, Mhe. Mchengerwa amewataka wataalam kuhakikisha miradi inazingatia mahitaji ya wananchi ili kuepuka miradi inayojengwa na kukamilika inaachwa bila kutumika kwa sababu ya kukosa ushirikishwaji wa wananchi, amewakumbusha kuwa miradi ya DMDP izingatie thamani ya mradi.
Akitoa salamu zake Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI Mhe. Jafari Wambura Chege amesema Kamati itaendelea kutoa ushirikiano kwa Mhe. Waziri ili waweze kuendelea kutatua kero za wananchi zinazowakabili katika maeneo yao kupitia Afya, Elimu na Miundombinu.
Post a Comment