WAZIRI BASHE AZINDUA KIUATILIFU HAI CHA KUANGAMIZA WADUDU DHURIFU WA MAZAO YA MAHINDI NA PAMBA


WAZIRI wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe (Mb) amezindua kiuatilifu hai cha kuangamiza wadudu dhurifu kwenye mazao (THURISAVE - 24) kilichovumbuliwa na kampuni ya Tanzania Biotech Products Limited (TBPL) leo tarehe 4 Oktoba 2024, mkoani Pwani.

Kiuatilifu hicho cha Thurisave kinadhibiti wadudu waharibifu wa zao la pamba na kantangaze kwenye nyanya. Kiuatilifu kinachodhibiti mbu ni aina nyingine ambacho pia kinatengenezwa na kampuni hiyo ya TBPL.

Wakati wa hotuba yake, Waziri Bashe amezielekeza Wizara ya Kilimo, Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) na Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) kuangalia uwezekano wa kuwa na makubaliano ya ushirikiano na Kampuni ya TPBL katika tafiti na uzalishaji wa viuadudu vya wadudu waaribifu wa mazao.

“TPHPA pia iangalie uwezekano wa kununua kiuatilifu hiki cha (THURISAVE - 24) na kusambaza bure kwa wakulima wa pamba na mahindi,” ameelekeza Waziri Bashe. Aidha, ameielekeza zaidi TPHPA ifanye utafiti ili kuweza kuangalia uwezekano wa kuwa na kiuatilifu hai kwa ajili ya zao la parachichi ambalo linazalishwa zaidi mikoa ya Njombe, Mbeya, Iringa, Kilimanjaro na mingine.

Kiwanda cha TBPL ni kiwanda cha Serikali chini ya usimamizi wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), ambapo kina thamani ya Dola za Marekani zaidi ya milioni 24 na ni kiwanda pekee barani Afrika kinachozalisha viuadudu vya kuangamiza mazalia ya mbu hususan kwenye mazao ya mahindi na pamba.

Aidha, hafla hiyo imehudhuriwa pia na Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Mhe. Abubakar Kunenge, Viongozi wa Taasisi za TPHPA, TARI na Viongozi wa Kampuni ya Tanzania Biotech Products Limited (TBPL).














0/Post a Comment/Comments