********
Na WAF, Dodoma
Mkurugenzi wa Sera na Mipango Wizara ya Afya, Bw. Amoury Amoury, amesema mpango wa Serikali wa kutekeleza Bima ya Afya kwa Wote utasaidia kudhibiti ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza na kuwezesha wananchi kumudu gharama za matibabu.
Bw.Amoury amebainisha hayo Novemba 14, 2024 Jijini Dodoma katika wiki ya magonjwa yasiyoambukiza katika kikao kazi cha kujadili mikakati ya kupambana na magonjwa yasiyoambukiza nchini, ambacho kimehusisha Wizara 15 za kisekta pamoja na wadau mbalimbali.
Bw. Amoury amesema kuwa, bima ya afya itawasaidia wananchi kudhibiti ongezeko la magonjwa yasiyoambukiza na kila mwananchi atapata huduma za uchunguzi pamoja na matibabu pale atakapozihitaji bila kikwazo cha fedha.
“Sheria hii ya bima ya afya kwa wote pia itamkinga mwananchi kulipia huduma ambazo zinaweza kumsababishia umaskini ambapo tumeshudia baadhi ya wananchi wasio na bima ya afya wakiuza mali ili waweze kugharamia matibabu,” amesema Bw. Amoury.
“Wananchi walio na bima ya afya hadi sasa ni asilimia 15, asilimia 85 ya wananchi hugharamia matibabu kwa malipo ya papo kwa papo,” amebainisha Bw. Amoury.
Aidha, ameeleza sheria ya Bima ya Afya kwa Wote inaweka ulazima kwa kila mwananchi kuwa na bima ya afya ambayo itawezesha kila mwanachi
kutibiwa na kuondoa dhana na mazoea yaliyopo ambapo mgonjwa huenda hospitali pale anapokuwa katika hali mbaya.
“Kwa kuwa na bima ya afya mwanachi ataenda hospitali mapema kabla ya kuwa na tatizo kubwa la ugonjwa na hivyo kutibiwa mapema na kuokoa gharama kubwa ambazo zingetumika kutibu ugonjwa ukiwa katika hali mbaya,” ameongeza Bw. Amoury.
Post a Comment