DCEA YAKAMATA KILOGRAMU 1,066.105 ZA DAWA ZA KULEVYA

                  *************

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imefanya operesheni katika maeneo mbalimbali nchini kati ya Oktoba na Novemba 2024, na kufanikiwa kukamata kilogramu 1,066.105 za Dawa za kulevya, mililita 447 za Dawa tiba zenye asili ya kulevya na kuteketeza jumla ya ekari 157.4 za mashamba ya bangi na lita 19,804 za kemikali bashirifu, huku watuhumiwa 58 wakikamatwa.


Hayo yamebainishwa leo Novemba 12, 2024 na Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) Aretas Lyimo akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

"Kati ya Dawa hizo, kilogramu 687. 32 za Skanka na kilogramu Moja (01) ya hashishi zilikamatwa eneo la Goba, Dar es Salaam, zikiwa na zimefichwa ndani ya nyumba ya mtuhumiwa," amesema Kamishna Jenerali Lyimo.

Kwamba uchunguzi umebaini kuwa wateja wengi wa Skanka ni Wanawake ambao hudai kutumia Dawa hizo kupunguza msogo wa mawazo na kujistarehesha.

Vile vile hashishi ambayo hutengenezwa kwa mchanganyiko wa maua na mafuta ya mbegu za bangi, inapovutwa huzalisha kemikali hatari zinazoweza kusababisha magonjwa ya akili kwa haraka ambapo ameeleza kuwa mara nyingi Jamii huamini kuwa watu wanapopatwa na magonjwa haya wamerogwa.

Kamishna Jenerali Lyimo amebainisha kuwa katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Mamlaka ilikamata mililita 120 za Dawa za tiba zenye asili ya kulevya aina ya Codein, zikiwa zinasafirishwa kwenda nje ya Nchi, pamoja na mililita 327 zilizokutwa nyumbani kwa mtuhumiwa eneo la Tabata Kinyerezi.

Amebainisha kuwa dawa hizo ziliingizwa nchini kinyume na taratibu, zikiwa zimewekwa chapa bandia ya dawa za kuogeshea mbwa na paka ili kuepuka kubainika.

Amesema kukamatwa kwa Dawa hizi ni ishara ya uwepo wa tatizo la matumizi holela ya dawa za tiba zenye asili ya kulevya ambapo hali hiyo inachangiwa na kuimarika kwa udhibiti wa dawa za Kulevya na kusababisha wafanyabiashara na watumiaji kutumia Dawa tiba ya kulevya kama mbadala wa dawa za Kulevya.

Ameeleza mkoani Dodoma, Mamlaka imewakamata watuhumiwa wawili Suleiman Mbaruku Suleiman (maarufu Nyanda), mwenye umri wa Miaka 52, na Kimwanga Msobi Lazaro (Miaka 37) wakazi wa Mtaa wa Kinyali, Kata ya Viwandani.

Kwamba watuhumiwa walikamatwa na jumla ya gramu 393 za Haroein ambapo ameeleza kuwa Nyanda anafahamika kama kinara wa biashara ya dawa za Kulevya mkoani humo na amekuwa akifuatiliwa Kwa muda mrefu.

Amesema kupitia operesheni za Kanda, DCEA pia imekamata kilo 303.553 za bangi, gramu 103.8 za heroin, na kilo 63 za mirungi katika maeneo mbalimbali nchini.

Kwamba mafanikio hayo ni matokeo ya nia thabiti ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha kuwa tatizo la dawa za Kulevya linakomeshwa ili kulinda Afya na usalama wa Watanzania.























0/Post a Comment/Comments