HOSPITALI YA CHATO KINARA USAFI WA MAZINGIRA GEITA

******

Na Daniel Limbe,Chato

HOSPITALI ya wilaya ya Chato mkoani Geita imeibuka mshindi wa kwanza katika kampeni ya usafi na utunzaji wa mazingira huku kijiji cha mlimani kikivunja rekodi hiyo kwa miaka mitatu mfululizo.

Akikabidhi zawadi mbalimbali kwa washindi ikiwemo vyeti maalumu pamoja na fedha taslimu, Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya hiyo,Mandia Kihiyo,amewapongeza washindi hao kwa kuimalisha suala la afya za jamii kutokana na kuitikia ushauri wa wataalamu kwa lengo la kuepuka magonjwa ya kuambukiza.

Amesema hospitali ya wilaya hiyo,imefanikiwa kushika nafasi ya kwanza kati ya hospitali sita za mkoa wa Geita huku ikishika nafasi ya 23 kitaifa kati ya hospitali 102 zilizokuwa kwenye mpango huo.

Kwa upande wa vijiji, kijiji cha mlimani kata ya Muungano wilayani hapa, kimeibuka mshindi wa nane kitaifa na cha kwanza katika mkoa na wilaya ya Chato baada ya kuvishinda vijiji 274 vilivyokuwa kwenye mpango wa uboreshaji usafi wa mazingira,ujenzi wa vyoo bora,pamoja na kunawa mikono.

"Aidha halmashauri yetu imeshika nafasi ya nane kitaifa kati ya halmashauri 137 zilizoteuliwa kwenye ushindani huo"amesema Kihiyo.

Mganga mkuu mfawidhi wa hospitali ya wilaya hiyo,Dkt. Madili Sakumi, ameipongeza serikali kwa kutambua mchango mkubwa wa hospitali hiyo katika suala zima la kutunza usafi wa mazingira,matumizi bora ya vyoo na kunawa mikono.

Aidha ameahidi kuendelea kufanya vizuri zaidi katika nyanja zote ikiwemo huduma bora za matibabu na utunzaji wa mazingira ili kuifanya jamii itambue kuwa eneo hilo ni bora na kimbilio sahihi kwa afya za binadamu.

Akizungumza mbele ya Baraza la madiwani, mwenyekiti wa halmashauri hiyo,Christian Manunga, amewataka watumishi wa idara ya afya kuendelea kutoa elimu kwa umma katika suala zima la kuchimba na kutumia vyoo bora na kwamba ni aibu kwa karne hii familia kuishi pasipo kuwa na choo bora.

"Tuendelee kuwahamasisha wananchi wetu kutumia vyoo bora, maana kufanya hivyo inatusaidia kuepukana na magonjwa ya kuambukiza ikiwemo kipindupindu,watu waendelee kunawa mikono pasipo kusubiri magonjwa ya mlipuko na mazingira yote yawe safi wakati wote"amesema Manunga.

Ofisa afya na usafi wa mazingira wa wilaya hiyo, Fransisca Charles, amesema mpango mkakati wa halmashauri hiyo ni kuhakikisha inaondokana na matumizi duni ya vyoo na kwamba ifikapo mwaka 2030 kaya zote ziweze kutumia vyoo bora.

"Iwapo wananchi wote watajikita kwenye utunzaji bora wa mazingira,kutumia vyoo bora pamoja na kunawa mikono kwa usahihi, itasaidia sana kujikinga na magonjwa yasiyo ya lazima na tutakuwa tumeisaidia serikali kutumia gharama ndogo kuhudumia wagonjwa, badala yake fedha hizo zitasaidia kutatua changamoto zingine za kimaendeleo"amesema Fransisca.





                  Mwisho.

0/Post a Comment/Comments