TANZANIA ya viwanda itawezekana iwapo makampuni na mashirika mbalimbali ya ndani na nje ya chini yatawatumia vijana wanaohitimu kwenye vyuo vya ufundi stadi (VETA) kutokana na umahiri walionao katika ushindani wa soko la nchi wanachama wa Afrika mashariki.
Hatua hiyo inatokana na fedha nyingi zinazowekezwa na serikali kupitia Wizara ya Elimu na mafunzo ya ufundi kwa vijana wanaojiunga na elimu ya ufundi huku walezi na wazazi wakiwa na jukumu la kuwasimamia vijana wao katika malezi na makuzi bora.
Akizungumza kwa niaba ya mkuu wa wilaya ya Chato mkoani Geita,Louis Bura,kwenye mahafali ya tatu ya Chuo cha ufundi stadi (DVTC) wilaya hiyo,Ofisa tarafa ya Buzirayombo,Mpoki Mwakigonjola,amesema wazazi wanalojukumu kubwa kuhakikisha wanalinda maadili ya nchi hatua itakayosaidia kupata wahitimu bora wanaoweza kujiajiri na kuajiriwa.
Kadhalika amewataka vijana wote wanaohitimu mafunzo mbalimbali nchini kutunza nidhamu kuanzia kwenye familia, shuleni,vyuoni,kwenye ajira na hata kwa jamii inayowazunguka kwa madai kizazi bora kinaanzia familia husika.
Aidha amesema serikali inatambua changamoto mbalimbali zilizopo kwenye chuo hicho na kwamba baadhi yake tayari zimeanza kutatuliwa na kwamba zilizosalia zinaendelea kufanyiwa kazi ili kuhakikisha eneo hilo linakuwa kimbilio la wanafunzi na kinara wa taaluma kwa umma.
Mkuu wa chuo cha mafunzo ya ufundi stadi (DVTC) Chato, Rilian Mlimira, akisoma risala kwa mgeni rasmi,amebainisha mafanikio ya chuo hicho ikiwa ni pamoja kuongezwa kwa kozi kutoka saba hadi 10 zinazopatikana chuoni hapo.
Amezitaja kozi hizo kuwa ni Ufundi uashi,mabomba,magari,umeme,ushonaji,upishi,huduma,uchakataji wa samaki,kompyuta na udereva.
Kwa mujibu wa mkuu huyo,chuo hicho kina uwezo wa kudahili wanafunzi 600 huku akitaja waliofanikiwa kuhitimu mafunzo yao kwa mwaka 2024 ni 165 kati ya 187 waliosajiliwa mwaka wa kwanza wa masomo.
Hata hivyo ameiomba serikali kuongeza vitabu vya ziada na kiada, madarasa pamoja na mabweni kutokana na ongezeko la wanafunzi wanaojiunga na chuo hicho kila mwaka.
Baadhi ya wahitimu wa mafunzo ya ufundi Veta Chato wakitoa burudani wa wageni waliohudhuria mahafali hayo.
Mwisho.
Post a Comment