*******
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri wa Nishati wanaosimamia Mradi wa Kufua Umeme
wa Rusumo, Mhe. Dkt. Doto Biteko amesema kuwa mawaziri wa nchi za Tanzania,
Burundi na Rwanda wamekutana na kujadiliana kuhusu mradi huo ambao upo karibuni
kuzinduliwa.
“ Mradi umefikia asilimia
99.9 na vimebaki vitu vichache ili kuukamikisha, katika kikao cha Baraza
la Mawaziri kuhusu mradi tumekubaliana
kuwasilisha maombi yetu kwa wakuu wa nchi ili watakapota nafasi mwakani mwezi
wa pili waweze kuzindua mradi huu,” amesema Dkt. Biteko.
Ameendelea kusema kuwa kwa sasa nchini Tanzania mahitaji ya
juu ya umeme ni Megawati 1,800 na kuna uwezo wa kuzalisha Megawati 3,070 hivyo kuna ziada ya umeme.
Amesisitiza “ Kuwa na vyanzo vingi ya umeme maana yake
tunakuza uchumi wa nchi yetu, asilimia 52 ya umeme wote tunaozalisha unatumiwa
na wananchi na asilimia 48 inatumika kwenye viwanda.”
Dkt. Biteko ametaja manufaa ya mradi huo kuwa hadi sasa
umezalisha ajira kwa watu pamoja na kusaidia uwepo wa miradi mbalimbali kwa
ajili ya huduma kwa jamii (CSR) hususan katika Halmashauri ya Ngara. Aidha,
mradi huo umeiunganisha Tanzania na nchi za Rwanda na Burundi na pia unatoa
fursa ya kuziuzia umeme nchi hizo endapo zitahitaji licha ya uwepo wa megawati
27 zinazopatikana kwa kila nchi.
Katika hatua nyingine, Dkt. Biteko ametoa wito kwa jamii
kuutunza mradi huo ili uweze kuendelea kutoa umeme “ Mradi huu hauwezi kuwa wa
kudumu kama hatutunzi mazingira na leo
tumetoa maelekezo kwa Baraza tuanze kupanda miti katika eneo la mradi ili
kuendelea kutunza mazingira na kuwa na vyanzo vya uhakika vya umeme,”
Imeelezwa kuwa, mradi wa huo wa kufua umeme unaotokana na
maji wa Rusumo, umeanza kuzalisha megawati 80 ambazo zinagawanywa kwa usawa wa
megawati 27 kwa nchi ya Tanzania, Rwanda na Burundi na hivyo kuzidi kuimarisha
gridi za Taifa za umeme.
Mradi huo unaotekelezwa na Kampuni ya Umeme ya Rusumo (RPCL)
inayomilikiwa na nchi zote tatu ni kielelezo cha azma ya Serikali ya Tanzania
kuhakikisha kuwa nchi inakuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika kwa ajili ya
shughuli za maendeleo na kijamii.
MWISHO
Post a Comment